Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Machi 19, 2024 Local time: 11:45

Polisi Uingereza yachunguza shambulizi la kigaidi nje ya msikiti


Ramani ya Msikiti ulioko eneo la Finsbury Park, London
Ramani ya Msikiti ulioko eneo la Finsbury Park, London

Polisi mjini London wamesema gari la kubeba bidhaa limewagonga watembea kwa miguu nje ya msikiti mapema Jumatatu, na kuwajeruhi watu 10.

Kwa mujibu wa vyombo vya dola shambulizi hilo linashughulikiwa kama ni kitendo cha ugaidi.

Naibu Kamishna Neil Basu, mratibu wa juu wa taifa katika kupambana na ugaidi, amewafafanulia waandishi Jumatatu kuwa mtu mmoja ametangazwa kupoteza maisha katika eneo la tukio huko kaskazini ya London.

Mtu huyo alikuwa tayari anapokea matibabu wakati wa shambulizi na ilikuwa mapema kusema iwapo kifo chake kinahusiana na tukio hilo.

Vyombo vya dola vimesema maafisa walimkamata dereva wa gari hilo mwenye umri wa miaka 48, ambaye alikuwa anashikiliwa na wananchi katika eneo la tukio.

Basu amesema inaelekea kuwa mtu huyu ndiye mshambuliaji pekee. Amewapongeza wale waliomzuilia asikimbie, na kusema hatua ya kumzuia inastahili pongezi.

Hatua hii inanithibitishia kuwa wakazi wa London watashirikiana kujilinda, lakini watafanya hivyo katika njia ambayo haiwafanyi waagukie katika mikono ya magaidi au wenye misimamo mikali,” Basu amesema.

Amesema kuwa watu 10 walijeruhiwa katika jamii ya Waislamu, na kuwa wachunguzi “wako tayari kusikiliza” kile kilicho wasukuma kufanya shambulizi.

Waziri Mkuu Theresa May amesema lile lililotokea Jumatatu lilikuwa “shambulizi dhidi ya Waislamu karibu na eneo lao la ibada,” na kuwa “chuki na ouvu wa namna hii hauwezi kufanikiwa.”

Harun Khan, katibu mkuu wa Baraza la Waislam Uingereza, amesema kutokana na taarifa za walioshuhudia tukio hilo dereva alikuwa amesukumwa na “chuki dhidi ya Uislam.”.

“Kwa kuwa tunakaribia mwisho wa mfungo wa Ramadhan na sherehe za Eid ambapo Waislamu wengi watakuwa wanaenda katika misikiti ya maeneo yao, tunategemea vyombo vya dola kuongeza ulinzi nje ya misikiti ikiwa ni jambo la dharura,” Khan amesema katika tamko lake.

Tamko lililotolewa na kituo cha Polisi ya Metropolitan limesema kuwa kutokana na hali hiyo ya shambulizi, “ulinzi wa ziada umeongezwa ili kuzihakikishia usalama jamii hizi na hasa wale wanaoshiriki katika mfungo wa ramadhani.

Uingereza, hasa London, imefikwa na matukio kadhaa hivi karibuni, likiwemo lile la kigaidi la mwezi uliopita ambapo bomu liliripuliwa Manchester na shambulizi la gari kugonga watu hivi karibuni na pia watu kuchomwa visu karibu na daraja la London.

XS
SM
MD
LG