Kamati yakutana
Spika wa Bunge Job Ndugai ameeleza: "Kama mnavyojua hapa Bungeni angalau tunaweza kujadili jambo baada ya kamati kulifahamu kwa undani wake. Nashukuru sasa kamati imeshaanza kuchukua hatua za kulifuatilia kwa ukaribu."
Kwa mujibu wa duru za habari wananchi katika maeneo yaliokumbwa na mauaji haya wamekuwa wakiishi kwa wasiwasi na hofu kubwa na wakihofia maisha yao na mali zao.
Maeneo hayo ni ya Mkoa wa Pwani ikiwemo Mkuranga, Kibiti, na Ikwiriri. Suala hilo tayari vyombo vya usalama nchini vimeanza kulishughulikia kwa mujibu wa spika ilikuhakikisha usalama wa raia na mali zao.
Kuuawa kwa askari
Katika tukio la hivi karibuni polisi wanane waliuawa na watu wanaodaiwa kuwa majambazi wilayani Kibiti mwishoni mwa wiki iliopita.
Hata hivyo spika amewataka wabunge kuwa watulivu na kusubiri ripoti ya kamati hiyo.
Muongozo kutoka kwa Mbunge
Spika alikuwa akijibu muongozo wa Mbunge wa Bukombe (CCM) Dotto Bitteko Bungeni. Mbunge huyo pamoja na wengine waliomba muongozo wa spika wakitaka kuahirishwa kwa Bunge ili liweze kujadili hali ya amani ya nchini kufuatia mauaji ya askari wa jeshi la polisi.
Hata hivyo spika alitumia hekima kuwasihi wabunge wawe watulivu wakati vyombo vyote vya ulinzi vikichukua hatua ya kukabiliana na hali ya uvunjifu huo wa amani nchini.
Historia fupi ya mauaji
Akitoa maelezo zaidi Mbunge Bitekko alisema kuwa: "Askari wetu wanane waliuawa na watu wanaodhaniwa ni majambazi, askari hawa walikufa wakiwa wanatekeleza majukumu ya kutulinda sisi raia pamoja na mali zetu."
"Tukio hili Mheshimiwa Spika sio tukio la kwanza kwenye eneo la Kibiti. Tukio hili liliwahi kutokea tarehe 21.0.2017, ambapo watu watatu waliuawa akiwemo mkuu wa upelelezi wa wilaya ya Kibiti, Peter Kubezya."
Hofu kwa wananchi
Bitekko ameeleza kuwa wananchi wa Tanzania kwa sasa kwa matukio haya yanayotokea wanahofu na usalama wao, na maisha yao na mali zao kutokana na matendo haya.
"Ninaomba kutoa hoja tuahirishe Bunge tuweze kujadili jambo hili," alisema Bitekko.
Kauli hiyo pia iliungwa mkono na wabunge wenzake ambao pia walieleza wasiwasi wao juu ya mauaji hayo na kutaka hatua za haraka zichukuliwe kujadili mustakbali wa jambo hili.