Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Aprili 19, 2024 Local time: 09:49

Uingereza yawashikilia watu wanane kufuatia shambulizi nje ya Bunge


Waziri Mkuu Theresa May
Waziri Mkuu Theresa May

Askari nchini Uingereza wamesema Alhamisi kuwa wanawashikilia watu wanane kufuatia shambulizi lililofanyika karibu na Bunge la Uingereza huko London, ambalo limeuwa watu watatu na kusababisha afisa kumpiga risasi na kumuua mshambulizi huyo.

Mark Rowley, kiongozi wa kampeni ya kupambana na ugaidi ya Kituo cha Polisi cha jijini London, amesema kamata kamata hiyo ilifuatia upekuzi katika anuani za wakazi sita.

Hata hivyo mahojiano yanaendelea kufanyika katika maeneo mbali mbali ya Uingereza, ikiwemo Birmingham na sehemu nyingine. Lakini hakubainisha vipi wale waliokamatwa wamehusishwa na shambulizi hilo la Jumatano.

“Bado tunaamini, na inazidi kujitokeza katika uchunguzi wetu, kwamba mshambuliaji alifanya hili peke yake na kuhamasishwa na ugaidi wa kimataifa,” Rowley amewaambia waandishi. Ameongeza kuwa mtu aliyefanya shambulizi jina lake halitakiwi kuwekwa wazi katika kile alichosema ni “hatua nyeti” ya uchunguzi huo.

Uchunguzi hivi sasa umejikita katika kuangalia kusudio, maandalizi na washirika wa mtu huyu aliyetumia gari kuwagonga watembea kwa miguu katika Daraja la Westminster, halafu kumpiga kisu afisa wa ulinzi na kumuua kabla yeye mwenyewe kupigwa risasi na afisa mwengine wa ulinzi.

Rowley amesema watu 29 wamelazwa hospitali, saba kati yao wako katika hali mbaya. Amesema watu ambao hawakuomba kupewa matibabu baada ya shambulizi hilo haijulikani.

Rowley mapema alimtambulisha afisa usalama aliyeuawa katika shambulizi hilo ni Keith Palmer mwenye umri wa miaka 48, ni mume na baba ambaye ametumikia katika vyombo vya ulinzi vya Uingereza kwa miaka 15.

Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa May ametoa kauli ya ushupavu, akisema watu wanatakiwa kuendelea na shughuli zao kama kawaida.

“ Watu wataendelea kupanda treni, watatoka nje ya hoteli wanakoishi, wataendelea kutembea mitaani, wataendelea kuishi maisha yao na sote tutasonga mbele pamoja, kamwe hatutojisalimisha katika vitisho vya ugaidi na katu hatutakubali kauli za chuki na maovu kuruhusu vitugawanye,” May amesema.

Jengo la Bunge limefunguliwa Alhamisi na wabunge waliomboleza kwa ukimya wa dakika moja kuwakumbuka wale waliouawa katika shambulizi. Maafisa wa Polisi pia waliomboleza, kwa kukaa kimya nje ya makao makuu ya polisi London iliyoko karibu na jengo la Bunge.

Serikali imeongeza ulinzi London wakati askari wenye silaha na wasio na silaha wakilinda doria kila mahali.

XS
SM
MD
LG