Msemaji wa polisi wa eneo hilo, Mohammad Asif Waziri, aliiambia Sauti ya Amerika kuwa mlipuko huo ulilenga sherehe ya kuheshimu vyombo vya habari vya Afghanistan katika mji mkuu wa jimbo hilo, Mazar-i-Sharif.
Alisema wanahabari watano na watoto watatu ni miongoni mwa waliojeruhiwa. Viongozi wa mkoa na wale wa kidini pia walikuwa miongoni mwa wageni waliohudhuria hafla hiyo.
Abdul Nafi Takor, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Ndani inayoongozwa na Taliban katika mji mkuu wa Afghanistan, Kabul, alisema kilipuzi kilichotegwa kilisababisha mlipuko huo.
"Nilisikia kishindo kikubwa ... kisha kukawa na hali ya sintofahamu huku kila mtu akijaribu kutafuta njia ya kutoroka," mwandishi wa habari wa Afghanistan. Atif Arian, aliyejeruhiwa katika mlipuko huo, aliliambia shirika la habari la AFP.
"Baadhi ya waandishi wa habari wamejeruhiwa vibaya," Arian aliongeza. Kituo kikuu cha runinga cha Afghanistan, TOLOnews, kiliripoti kuwa mmoja wa wanahabari wake alikuwa miongoni mwa waathiriwa.
Hakuna aliyedai mara moja kuhusika na shambulio hilo, ambalo limetokea siku mbili baada ya mshambuliaji wa kujitoa mhanga kumuua gavana wa jimbo la Balkh, Mohammad Dawood Muzammil, katika afisi yake kwenye mji wa Mazar-i-Sharif, pamoja na watu wengine wawili.