Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Februari 27, 2024 Local time: 02:53

Tanzania yasisitiza kuvujisha takwimu kosa la jinai


Dkt Philip Mpango
Dkt Philip Mpango

Serikali ya Tanzania imeonya kuwa wadadisi  watakaovujisha siri za takwimu watakazokusanya za mapato na matumizi ya kaya binafsi, watashtakiwa na kufikishwa mahakamani.

Kauli hiyo imetolewa Jumamosi na Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt Philip Mpango akiwatahadharisha wadadisi watakao husika na zoezi hilo kuwa kuvujisha siri hiyo ni kosa la jinai kwa mujibu wa sheria ya Takwimu ya mwaka 2015.

Vyanzo vya habari nchini Tanzania vimesema kuwa aliwataka wananchi wote nchini ambao kaya zao zimechaguliwa kushiriki katika utafiti huo, kuhakikisha wanatoa taarifa sahihi za kila mwanakaya wa kuanzia umri wa miaka mitano na kuendelea.

Wadadisi hao watakwenda kufanya utafiti na kukusanya takwimu za kaya binafsi 10,460 katika Tanzania Bara kuanzia Novemba 2017 huu hadi Novemba 2018.

Utafiti huo utaiwezesha serikali kupima kiwango cha hali ya umasikini wa kipato, chakula na pengo baina ya matajiri na masikini kuanzia kipindi cha mwaka 2013 hadi sasa na kutaiwezesha serikali kutathmini hatua zilizofikiwa katika kutimiza malengo ya kitaifa yaliyoanishwa katika Mpango wa Pili wa Maendeleo wa miaka mitano (2016/17-2020/21) na malengo ya Maendeleo Endelevu 2030.

Utafiti kama huo uliyowahi kufanyika siku za nyuma, umeonyesha kwamba kiwango cha umasikini wa kipato kinaendelea kupungua kutoka asilimia 34 mwaka 2007 hadi kufikia asilimia 28.2 mwaka 2011/12.

Serikali imesema pamoja na mafanikio hayo, changamoto za maendeleo bado zipo na ndiyo maana inaendelea kushirikiana na wananchi na wadau wengine katika juhudi za kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma za msingi za kijamii kadiri uchumi unavyokua na hivyo kupunguza kama si kumaliza kabisa na umasikini.

XS
SM
MD
LG