Matokeo yaliyotolewa kufikia sasa kufuatia uchaguzi wa Desemba 20 yanamuonyesha Rais Felix Tshisekedi akiongoza dhidi ya wapinzani wake. Mvutano hata hivyo unaongezeka kuhusu uchaguzi huo ambao unatishia mukstkabal wa taifa la DRC, ambalo bado linakabiliana na mzozo wa usalama katika maeneo ya mashariki. Kongo ndio mzalishaji mkuu wa cobalti, vyuma, na madini mengine ya kiviwanda.
Maafisa wa usalama waliwakabili waandamanji na kuzima maandamano yaliyopigwa marufuku siku ya Jumatano katika mji mkuu Kinshasa na watu waliokuwa wakipinga jinsi uchaguzi wa rais na wabunge ulivyoendeshwa. Upinzani umesema kulikuwa na kasoro nyingi na udanganyifu. Tume ya uchaguzi CENI inakanusha hili.
Msemaji wa serikali Patrick Muyaya alisema kuwa upinzani unapaswa kusubiri hadi matokeo kamili yatakapochapishwa na kuyapinga katika mahakama ikibidi.
Kundi la Moise Katumbi, mmoja wa wapinzani wakuu wa Tshisekedi, limefutilia mbali matumizi ya njia za kisheria kupinga matokeo, likisisitiza kwamba taasisi za serikali zilihusika katika undanganyifu wa kura kwa kumpendelea rais na kusema uchaguzi unapaswa kubatilishwa. Vyama vingine vya upinzani vimetoa wito wa kurudiwa kwa kura hiyo.
Muyaya alisema serikali imejitolea kufanya mchakato wa uchaguzi wa haki na wa uwazi na akatupilia mbali tishio la Katumbi la kufanya maandamano zaidi kote nchini.
CENI inatazamiwa kutoa matokeo zaidi ya muda ya urais kabla ya tarehe ya mwisho ya Desemba 31. Matokeo ya hivi punde yalionyesha Tshisekedi akiwapita wapinzani wake 18 kwa zaidi ya 77% ya kura zilizopigwa milioni 9.3 na kuhesabiwa kufikia sasa.
Upinzani na waangalizi wa kujitegemea wanahoji uhalali wa matokeo haya, wakiishutumu CENI kwa kushindwa kufuata utaratibu sahihi wa ujumlishaji na uchapishaji wa matokeo, pamoja na utata uliojitokeza siku ya uchaguzi.
Forum