Watoto hao walikuwa tayari katika mchakato wa kutumikishwa kibiashara na nyumbani wilayani Kahama na Shinyanga.
Taarifa hiyo ilitolewa katika kilele cha maadhimisho ya Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia na dhidi ya watoto, yaliyofanyika katika Halmashauri ya Mji wa Kahama, nchini Tanzania.
Vyanzo vya habari vimeeleza kuwa taarifa ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Anderson Msumba, ilifafanua kwamba watoto 360 walikutwa wakisafirishwa kutoka Burundi, 20 kutoka Rwanda na 20 wengine kutoka mikoa ya Ngara na Kigoma, Tanzania.
Serikali tayari imechukua hatua ya kuwarejesha watoto hao kwa familia zao, huku wasafirishaji haramu wakifikishwa kwenye vyombo vya sheria.
Katika kipindi hicho pia wasichana 27 walikatishwa masomo kwenye shule mbalimbali za msingi Kahama baada ya kupata mimba.
Kwa mujibu wa Ofisa Maendeleo ya Jamii wa Wilaya ya Kahama, Mary Cluma, kumekuwepo mila, desturi na tamaduni potofu zikiwemo za wazazi na walezi kuozesha mabinti wadogo ili kujipatia mali.