Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Oktoba 08, 2024 Local time: 08:25

Ruto avilaumu vyombo vya habari, adai vinaegemea zaidi kwa Odinga


William Ruto
William Ruto

...Bw Ruto ndiyo amedai kuwa  vyombo vya habari vya nchini humo vimekuwa vikiegemea sana kwa Bw Odinga licha ya ripoti ya Julai mwaka 2022 ya Baraza la Vyombo vya Habari nchini Kenya kuonyesha kuwa Bw Ruto ameangaziwa sana kumpiku Bw Odinga na wagombea wengine.

Huku uchaguzi wa Agosti 9 nchini Kenya ukikaribia na kuonekana kuwa na ushindani mkubwa, vyombo vya habari vinaendelea kutupiwa lawama kwa kuonyesha upendeleo kwa baadhi ya wagombea, suala linalotajwa kuwa la makusudi na kambi za upinzani.

Raila Odinga
Raila Odinga

Licha ya wagombea wa urais nchini Kenya kuwa wanne pekee; William Ruto wa United Democratic Alliance, Raila Odinga wa Azimio la Umoja One Kenya, Prof George Wajackoyah wa Roots Party na David Waihiga Mwaure wa Agano Party, ni Bw Ruto ndiyo amedai kuwa vyombo vya habari vya nchini humo vimekuwa vikiegemea sana kwa Bw Odinga licha ya ripoti ya Julai mwaka 2022 ya Baraza la Vyombo vya Habari nchini Kenya kuonyesha kuwa Bw Ruto ameangaziwa sana kumpiku Bw Odinga na wagombea wengine.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya ufuatiliaji wa viwango vya matangazo yanayowaangazia wagombea wa urais, mpeperushaji wa bendera ya United Democratic Alliance, William Ruto, amepokea kiwango cha juu cha matangazo yanayomwangazia na sera zake hasa baada ya kuzindua ilani yake ya uchaguzi.

Ripoti hiyo iliyowekwa wazi wiki ya kwanza ya mwezi Julai, inaonyesha kuwa matangazo yanayomuangazia Bw Ruto yanafikia asilimia 46 dhidi ya 45 ya Bw Odinga, huku George Wajackoyah na David Mwaure wakiwa na asilimia 6 na asilimia 3 mtawalia.

Takwimu zinaonyesha kuwa muungano wa Bw Ruto ulitajwa kwa asilimia 14 kwenye magazeti ikilinganishwa na asilimia 12 ya muungano wa Odinga na asilimia 61 ya matangazo ya redio dhidi ya 58 ya Odinga.

Pia inaashiria kuwa Ruto anaongoza katika utangazaji wa magazeti na redio, huku Odinga akiendelea kuongoza dhidi ya Bw Ruto kwenye matangazo ya televisheni kwa asilimia 29 dhidi ya 26 ya Bw Ruto.

Lakini kwenye takwimu za mwezi uliotangulia, utangazaji unaohusu Bw Odinga ulikuwa wa hali ya katika kipindi cha kabla na baada ya kuzinduliwa kwa ilani ya uchaguzi ya muungano huo. Na kuongoza kwa Bw Ruto katika upeperushaji wa matangazo kwenye vyombo vya habari ulikuwa wa juu vile vile baada ya uzinduzi wa manifesto yake.

Raila Odinga (kati), wakati akiwa kiongozi wa upinzani na mgombea wa urais wa chama cha National Super Alliance (NASA) mwaka 2017. REUTERS/Baz Ratner - RC11FFAE1930
Raila Odinga (kati), wakati akiwa kiongozi wa upinzani na mgombea wa urais wa chama cha National Super Alliance (NASA) mwaka 2017. REUTERS/Baz Ratner - RC11FFAE1930

Ripoti ya Baraza hilo vile vile ilionyesha kuwa angalau asilimia 49 ya wanahabari nchini Kenya wanajihisi salama wakiripoti kwenye kambi ya muungano wa Azimio la Umoja wa Bw Odinga, huku asilimia 31 wakijihisi salama kwenye muungano wa Bw Ruto.

Lakini hilo halijamfanya Bw Ruto kusita kuvilaumu vyombo vya habari kwa kile anachokitaja kuwa ni upendeleo wa wazi kwa Bw Odinga.

Hata hivyo, Victor Bwire, Naibu Mkurugenzi na Meneja wa Mipango wa Baraza la Vyombo vya habari nchini Kenya anaeleza kuridhishwa na utendaji wa vya vyombo vya habari kipindi hiki cha uchaguzi.

Aidha, Bw Bwire anaeleza kuwa iwapo kuna mapungufu katika matangazo yanayowaangazia baadhi ya wagombea, huenda ni matatizo ya baadhi ya vyombo vya habari husika lakini haliwezi kuwa suala la makusudi.

Rasimu ya Ripoti ya Kituo cha African Centre for Media Excellence inayoangazia ripoti za televisheni kwa wagombea hawa kati ya Mei na Juni, mwaka huu, inaonyesha kuwa televisheni ya Citizen ilipeperusha asilimia 59.6 ya taarifa zake zilizomuangazia Bw Odinga, Ruto kwa asilimia 36.0, Wajackoya asilimia 3.5 huku Mwaure akipokea asilimia 0.9; Wakati huo televisheni ya K24 ilipeperusha asilimia 60.6 ya taarifa zinazomwangazia Bw Odinga, Ruto kwa asilimia 37.9, Mwaure asilimia 1.5 naye Wajackoya hakuangaziwa kabisa; NTV na KBC Channel 1 zilipeperusha taarifa zinazomwangazia Bw Odinga kwa asilimia 56.8 na 56.7 mtawalia huku Bw Ruto akipokea asilimia 36.8 na 40.2 mtawalia. Mwaure na Wajackoyah waliangaziwa chini ya asilimia 1. Nayo KTN News ilipeperusha matangazo mengi ya Bw Odinga kwa asilimia 53.0, Ruto 36.3, Wajackoyah na Mwaure asilimia 4.3 kila mmoja. Kituo hicho kinahitimisha kwa kusema kuwa Bw Odinga anapata matangazo ya juu zaidi katika vituo vingi vya televisheni nchini Kenya licha ya takwimu nyingine kuonyesha ukaribu kati yake na Bw Ruto.

Dkt George Gathigi, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Nairobi anaeleza kuwa huenda sifa za wagombea zinachangia katika viwango vya matangazo yanayopeperushwa.

Dkt Gathigi, aidha anakariri kuwa vyombo vya habari wakati wote vinastahili kuendeleza viwango vya juu vya taaluma na kuripoti uchaguzi kwa ukamilifu.

Bw Odinga bado ndiye mgombeaji urais anayependwa zaidi kwa asilimia 46.7 huku Bw Ruto akiwa na asilimia 44.4, Wajackoya kwa asilimia 1.8 naye Waihiga Mwaure kwa asilimia 0.1, kura mpya ya maoni ya shirika la Tifa inaonyesha.

Kura ya Center for African Progress inamuweka Bw Odinga akiwa na asilimia 52 na Dkt Ruto akiwa na asilimia 45.

Imetayarishwa na mwandishi wetu Kennedy Wandera, Nairobi.

XS
SM
MD
LG