Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Mei 24, 2024 Local time: 23:52

Wasifu wa mgombea urais Kenya Prof. George Luchiri Wajackoya


Prof George Luchiri Wajackoyah, mgombea urais nchini Kenya. Picha: George Wajackoyah twiter page
Prof George Luchiri Wajackoyah, mgombea urais nchini Kenya. Picha: George Wajackoyah twiter page

Prof. George Luchiri Wajackoyah ni mwanasiasa na mgombea urais katika uchaguzi wa Kenya wa mwezi Agosti. anataka kuhalalisha bangi. Amejizolea umaarufu kwa mda mfupi Sana ikilinganishwa na wanasiasa wengine wanaogombea nafasi ya urais ambao wamekuwa katika siasa za Kenya kwa mda mrefu sana.

Maisha yake ni mchanganyiko wa masumbuko wa kimaisha, umaskini uliokithiri na ufanisi. Labda Wajackoya ndiye mkenya aliyesoma zaidi kufikia sasa kutokana na shahada zake kadhaa.

Aliishi Maisha ya kurandaranda mitaani, akiwa mtoto kwa kuomba omba mitaani, alifanya kazi kama bawabu, mchimba makaburi, mhubiri wa injili, wakili, profesa wa sheria, mwanasiasa na sasa mgombea wa nafasi ya juu zaidi katika uongozi wa Kenya katika uchaguzi mkuu wa mwezi Agosti 2022.

Profesa Luchiri Wajackoya ana shahada 16. Ana uwezo wa kuzungumza lugha 11. Amejizolea umaarufu sana kutokana na sera yake ya kutaka kuhalalisha kilimo na uuzaji wa bangi endapo atachaguliwa kuwa rais wa Kenya.

Maisha ya wajackoya

Prof Wajackoyah alizaliwa mwezi Oktoba tarehe 24 mwaka 1959. Katika mahojiano na Sauti ya Amerika, alisema kwamba alizaliwa mjini Jinja Uganda. Wazazi wake ni raia wa Kenya.

Babake ni Tito Olilo Jakoya, mzaliwa wa Mumias, Kaunti ya Kakamega.

Mamake ni Melenia Makokha, mzaliwa wa Muluanda, samia, wilaya ya Busia, Kenya.

Wazazi wake Wajackoya walitalakiana akiwa bado mtoto mchanga na aliishi na wazazi wa baba yake.

Wajakoya Polisi na mpelelezi makosa ya jinai

Alihamia Nairobi akiwa na umri wa miaka 16, baada ya kumaliza masomo ya shule ya msingi. Aliishi kwa kutegemea wahisani kwenye barabara za jiji la Nairobi kabla ya kuchukuliwa na jamii ya wahindi, na hata kupewa jina la Balaram.

Alilipiwa karo ya shule ya upili na jumuiya ya wahindi aliokuwa anaishi nao. Alisomea shule ya upili ya St Peters Mumias na kumaliza masomo ya shule ya upili mwaka 1980.

Alisajiliwa kwa mafunzo ya polisi katika chuo cha polisi cha Kiganjo.

Alifanya kazi kama afisa wa polisi hadi akafikia ngazi ya inspector.

Alipewa majukumu ya kukusanya Ushahidi kuhusiana na kifo cha aliyekuwa waziri wa mambo ya nje wa Kenya Robert Ouko.

Mambo yalimgeukia kutokana na Ushahidi aliokuwa anakusanya na akakamtwa, akawekwa kizuizini bila kufikishwa mahakamani na kuteswa.

Aliambia Sauti ya Amerika kwamba kuna raia wa Marekani walimsaidia na kumtoa kizuizini. Hakutaka kuwataja waliomsaidia.

Alitorokea Uingereza mwaka 1990 baada ya kutoka kizuizini kwa sababu hakujihisi salama nchini mwake.

Shahada za Wajackoya

Akiwa Uingereza, Waajackoya alijiunga na chuo kikuu cha Wolverhampton, mjini London kwa masomo ya juu.

Alijongezea masomo na kupata shahada kadhaa katika vyuo vikuu vya Warwick, Westminster na UOL Birkbeck.

Alikuwa anachimba makaburi mchana huku akiwa bawabu usiku ili kulipa karo.

Ana shahada kadhaa katika masomo ya sheria kutoka vyuo vikuu mbalimbali. Amesoma pia lugha ya kifaransa, masomo ya usalama na uchunguzi wa uhalifu wa jinai, uchumi, filosofia na masomo kuhusu Afrika.

Baada ya kupata shahada zake akiwa Uingereza alifungua ofisi na kufanya kazi kama wakili wa kuwasaidia wakimbizi na wahamiaji.

Aliishi Uingereza kwa miongo miwili akifanya kazi kama wakili kabla ya kuhamia Marekani.

Maisha ya Wajackoya Marekani

Akiwa Marekani, Wajackoya aliendeela kusoma sheria katika chuo kikuu cha Baltimore. Alifunza katika chuo kikuu cha American Heritage, California.

Alirudi Kenya mwaka 2010 na kufungua ofisi yake ya sheria kwa jina Luchiri & Co. Advocates.

Alitangaza kugombea urais nchini Kenya mara ya kwanza mwaka 2012 lakini akajiondoa bila kutoa sababu yoyote.

Mwaka 2021, Prof Wajackoya alitangaza nia ya kugombea urais kwa chama cha Roots, katika uchaguzi wa mwezi Agosti tarehe 9 mwaka 2022. Kura za maoni zinamueka katika nafasi ya tatu nyuma ya Raila Odinga na Dr. William Ruto.

Chama chake cha Roots kinafanya kampeni ya kuhalalisha ukulima na uuzaji wa bangi nchini Kenya. Chama hicho kina amini kwamba kilimo cha bangi kina uwezo mkubwa wa kuimarisha uchumi wa Kenya na kuondolea nchi hiyo mzigo wa madeni.

Kando na siasa, Prof Wajackoya ni mhadhiri wa sheria ya kimataifa katika chuo kukuu cha kimataifa cha Marekani tawi la Afrika, USIU, jijini Nairobi. Pia ni mwanachama wa taasisi ya uhamiaji katika chuo kikuu cha Nairobi.

Familia ya Wajackoya

Prof Wajackoya ana mke na mtoto. Mke wake ni Mmarekani mwenye asili ya Kiafrika.

Wajackoya aliambia Sauti ya Amerika kwamba mke wake amekuwa naye katika safari yake ya magumu na yaliyo rahisi. Hata hivyo, hayupo tayari kuingiza familia yake katika siasa na hivyo majina ya mke na watoto wake yamesalia siri.

Amesema kwamba kila pesa amepokea inatokana na jasho lake kwa malipo kutoka kwa huduma ya uakili ambayo amefanya kwa kuwatetea wahamiaji baadhi wakiwa watu maarufu na wanasiasa Afrika mashariki.

Thamani ya Wajackoya kifedha haijulikani lakini anaaminika kuwa mtu Tajiri anayeishi Maisha ya kawaida.

Ukweli kumhusu Prof George Luchiri Wajackoya

 • Ana umri wa miaka 62 (24 Oktoba 1959)
 • Ni mkenya aliyezaliwa Uganda
 • Alikuwa mtoto wa kurandaranda mitaani
 • Aliwahi kuwa afisa wa polisi
 • Amesomea sheria
 • Ana shahada 16. Hakuna Mkenya mwingine anayejulikana kuwa na idadi ya shahada kama zake
 • Hana dini yoyote lakini anaamini katika ‘roho’. Anaamini kwamba Mungu ndiye hutangulia katika kila jambo
 • Ameoa. Ana mke mmoja na mtoto
 • Familia yake inaishi Marekani
 • Wajackoya ni mhadhiri katika chuo kikuu cha Marekani tawi la Afrika – USIU, Nairobi
 • Anagombea urais kupitia chama cha roots party

Imetayarishwa na Kennes Bwire, VOA, Washington DC

XS
SM
MD
LG