Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatano, Februari 01, 2023 Local time: 17:51

Polisi yauwa majambazi wanne, silaha mbili zilizoporwa zakamatwa


Mwigulu Nchemba

Polisi nchini Tanzania imewauwa watu wanne wanaosadikiwa kuhusika na mauaji ya askari polisi zaidi ya kumi katika eneo la Mkengeni, kata ya Mjawa, Wilaya ya Kibiti mkoani Pwani. Pia imetangaza uperesheni maalum katika eneo la Kibiti.

Jeshi la Polisi limetoa maelezo juu ya sababu ya kuwepo mauaji ya askari katika maeneo ya Mkuranga, Rufiji, Ikwiriri na Kibiti.

Limeeleza kuwa ni kwa sababu ya kuwepo mapori makubwa ambayo hutoa mwanya kwa watu wenye naia mbaya ya kutenda vitendo vya uhalifu kupata mahali pa kujificha.

Kamshina wa Operesheni na Mafunzo, Nsato Msanzya amesema jeshi hilo limeanzisha msako mkali baada ya vitendo vya mauaji hayo ya kinyama Alhamisi na itaendeleza operesheni maalum katika eneo la Kibiti.

Amesema kuwa katika mapambano na majambazi hao polisi wamefanikiwa kuzikamata silaha mbili kati ya saba zilizokuwa zimechukuliwa kutoka kwa askari waliouawa, zoezi ambalo lilifanyika katika eneo ambalo mauaji hayo yalifanyika.

Kamanda huyo amesema kuwa katika operesheni hiyo, ambapo kikundi cha upelelezi kilipelekwa mara moja katika eneo la tukio wapelelezi waliweza kugundua maficho ya muda ya majambazi hao na katika kutupiana risasi majambazi wanne waliuawa, aliongeza kusema.

Waziri wa Mambo ya Ndani

Kwa mujibu wa vyanzo vya habari Tanzania, Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba amesema matukio ya kihalifu ya aina hii hayajazoeleka na wala si ya kawaida nchini.

Alikanusha yale yalioripotiwa na vyombo vya kigeni kusema askari polisi kushambuliwa na kuporwa silaha ni kawaida nchini Tanzania.

Waziri amesema kuwa shambulio hilo ni la kulipiza kisasi kutokana na kazi nzuri inayofanywa na jeshi la Polisi katika kukabiliana na makundi ya kihalifu ambayo yanajificha ndani ya misitu katika maeneo ya Kibiti.

Amesema kutokana na matukio kadha katika maeneo hayo ya Kibiti, Polisi walianza kazi nzito ya kukabiliana nao na hivyo kitendo walichofanya usiku wa kuamkia jana ilikuwa ni kulipiza kisasi baada ya kusukumwa kutoka katika maeneo waliyozoea kukaa na kufanya shughuli zao za kihalifu.

Akiwa katika eneo la tukio, waziri Mwigulu ameongeza kuwa tukio lililotokea sio taarifa njema na ni jambo baya kwa Tanzania na Ukanda huo ambao umekuwa na matukio mengi ya mauaji.

Aliongeza kuwa tukio hilo limeifanya serikali kuangalia namna mpya ya kujipanga kukabiliana na matukio hayo ambayo yameendelea kugharimu maisha ya askari.

“Tutapambana kwa nguvu zote kuhakikisha uhalifu wa aina hii haupati nafasi katika ukanda huu na kanda nyingine na niseme tu wale wote waliohusika kufanya vitendo hivi hawatavumiliwa na tutahakikisha wanalipa, hatuwezi kukubaliana na tutahakikisha tunapambana kurudisha silaha zetu na kuwakamata wote waliohusika,”alisema Mwigulu.

Mkuu wa Mkoa wa Pwani

Naye Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Evarist Ndikilo amesema tukio hilo ni la kusikitisha na sio la kufumbiwa macho, limeripoti gazeti la habari leo nchini Tanzania.

Alisema katika kuhakikisha wanakabiliana na matukio hayo ofisi yake pamoja na Wizara ya Mambo ya Ndani watasajili upya wananchi wanaojishughulisha na uchomaji mkaa kwa kuwa matukio mengi yanayofanyika wahusika wanakimbilia katika maeneo ya wachoma mkaa.

“Tumeongea hapa na Waziri ili tuwasajili upya watu hawa wanaochoma mkaa kwakuwa wakiwa na leseni tutaweza kuwatambua na wale wataokimbia katika maeneo hayo baada ya kufanya matukio iwe rahisi kuwapata kwa kuwa baada ya tukio wamekuwa wakikimbilia katika maeneo hayo,”alisema.

Ndikilo pia amewataka wananchi wa maeneo hayo kuwa na tabia ya kushirikiana na jeshi la polisi ili kuhakikisha wanadhibiti uhalifu huo, kwani wananchi wengi wamekuwa wagumu kutoa ushirikiano kwa vyombo vya dola.

Alisema baada ya kutembelea eneo la tukio wamebaini wahusika walikaa katika eneo hilo zaidi ya siku tano kwa kuwa walikata baadhi ya miti ambayo tayari imekauka, hivyo kungekuwepo na ushirikiano baina ya wananchi na jeshi hilo wangeweza kupata taarifa mapema na kudhibiti tukio hilo.

“Bado tunajiuliza hatujui hawa wananchi wana hasira gani na jeshi la polisi wamekuwa hawatoi ushirikiano hata kama mhusika yupo katika eneo lake hatuelewi ni sababu za kisiasa au kiuchumi hatujui,” aliongeza Ndikilo.

Aidha Ndikilo ameliomba jeshi hilo kuongeza askari katika eneo hilo ambalo lina mapori makubwa ambayo hutoa mwanya kwa watu wenye nia mbaya kufanya matukio na kujificha.

Wananchi wajawa na hofu

Kwa mujibu wa wananchi wa eneo hilo wameelezea kujawa na hofu kubwa huku wengi wakihofia usalama wao.

Akizungumza na gazeti la Habari Leo lakini kwa sharti la kutotajwa jina lake mkazi wa eneo hilo alisema matukio hayo yamekuwa ni ya kujirudia, hivyo wameiomba serikali kuongeza nguvu katika eneo hilo.

“Naogopa hata kuzungumza na wewe nisije nikaonekana sababu hapa ukizungumza na waandishi wa habari wakikugundua wanakutolea vitisho na wengine hadi wanauawa."

"tunaomba sana jeshi la polisi kuhakikisha wanaongeza nguvu katika eneo hili kwa kuwa sasa tunaogopa sijui kama wakimaliza kwa askari watakuja kwetu,”alisema Mwananchi huyo.

XS
SM
MD
LG