Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumamosi, Julai 27, 2024 Local time: 04:54

'CUF ikikaidi amri itapambana na nguvu ya dola'


JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam limepiga marufuku mpango wa wanachama wa Chama cha Wananchi (CUF) waliokusudia kufanya usafi katika ofisi za Makao Makuu ya chama hicho yaliyoko Buguruni jijini Dar es Salaam kesho, kutokana na sababu za kiusalama.

Polisi pia imebainisha kuwa imewaita viongozi wa pande mbili za chama hicho, upande wa Profesa Ibrahim Lipumba na upande wa Maalim Seif ili kuwaeleza umuhimu wa kutii sheria na "kama wana ugomvi usitoke nje kwa kuwa ukitoka maana yake wanataka kupambana na nguvu ya dola."

“…hivyo mwana Dar es Salamu yoyote, naomba usishiriki katika shughuli hii kwa kuwa kuna dalili kuwa makundi haya yakikutana kutakuwa na fujo,” amesema Kamanda wa Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam.

Simon Sirro alitoa katazo hilo wakati akizungumza na waandishi wa habari Jumamosi akisema jeshi hilo lilipokea barua kutoka Ofisi ya Mbunge wa Jimbo la Temeke, Abdallah Mtolea ambaye ni mfuasi wa Maalim Seif, ya kuomba wanachama wa chama hicho kufanya usafi wa mazingira katika ofisi hiyo iliyopo Buguruni kesho.

Aliongeza kuwa kutokana na barua hiyo “Jeshi la Polisi Kanda Maalumu limezuia shughuli hiyo na kumfahamisha Mtolea kuwa kutokana na sababu za kiusalama pamoja na mgogoro wa muda mrefu unaoendelea ndani ya CUF.

“Jeshi limemshauri kuwa kila mwanachama au mwananchi afanye usafi katika eneo lake analoishi au ofisi anayofanyia kazi kwani kitendo cha wao kukusanyika kwa kigezo cha kufanya usafi kinaweza kusababisha uvunjifu wa amani,” amesema Sirro.

Katika hatua nyingine, Sirro amesema jeshi hilo linawashikilia watu saba kutokana na vurugu zilizotokea katika mkutano wa chama hicho uliofanyika Manzese, Dar es Salaam hivi karibuni. Kwa mujibu wa kamanda huyo watu hao tayari wamefunguliwa mashitaka na jalada lao limepelekwa kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ili kulipitia na kuandaa mashitaka kwa ajili ya kuwapeleka mahakamani.

Aliwataja baadhi ya watu waliokamatwa kuwa ni pamoja na Ofisa Uhusiano wa chama hicho Abdul Kambaya(47), mlinzi wa karibu wa Mwenyekiti wa upande mmoja wa chama hicho Profesa Ibrahim Lipumba aitwaye Mtawa Rashid (35) na Khamis Abdallah maarufu kama ‘Taekwondo’ (35). “Kimsingi waliokamatwa mpaka sasa ni saba upelelezi umefanyika vizuri tunasubiri Mwanasheria Mkuu wa Serikali apitie jadala ili hatua zaidi zichukuliwe,” alisema Sirro.

Aidha Sirro alisema kati ya watu waliokamatwa; wawili wamelalamika kujeruhiwa hivyo jeshi hilo limewahoji watu wanaodaiwa kuwajeruhi watu hao kutokana na malalamiko yao huku mmoja Mohamed Mgomvi alikimbia na jeshi hilo linaendelea na jitihada za kumpata.

XS
SM
MD
LG