Haya yamefichuliwa katika mkutano kati ya rais Yoweri Museveni na wabunge, walio eleza kwamba maafisa wa polisi wanadai kwamba kuwalinda wabunge kwa sasa ni sawa na kujitafutia kifo.
Vitisho dhidi ya wabunge
Hatua ya maafisa wa polisi wa Uganda kukataa kutoa ulinzi kwa wabunge inatokana na video inayosambaa kwenye mitandao ya kijamii nchini Uganda, ikiwaonya wabunge kutoka chama kinacho tawala cha NRM, kwamba watauawa, baada ya kuifanyia katiba ya nchi hiyo mabadiliko na kuondoa kizuizi cha umri kilichokuwa kina mbana rais Museveni kuwania muhula mwingine madarakani.
Video hiyo inajiri baada ya mauaji ya aliyekuwa mbunge wa manispaa ya Arua Ibrahim Abiriga.
Polisi waingiwa na hofu
Na baada ya kuthibitishwa kwamba maafisa wa polisi wameogopa kutoa ulinzi kwa wabunge, rais Yoweri Museveni amemwelekeza mkuu wa jeshi Generali David Muhoozi, kutoa ulinzi wa kijeshi kwa wabunge hao, na kutaka mkuu wa polisi Okoth Ochola kuwafuta kazi polisi ambao wamekataa kuwalinda wabunge. Kaps Fungaroo, ni mbunge wa upinzani aliyehudhuria kikao cha rais Museveni na wabunge siku ya jumatano, wakati hoja hiyo ilipojadiliwa.
“Polisi wanakimbia. Polisi wanasema kwamba badala ya kumlinda mbunge, ni afadhali afutwe kazi. Wanasema kwamba kuwasindikiza wabunge inahatarisha maisha yao. Na rais Museveni ameamurisha kwamba polisi wanaokataa kuwalinda wabunge wafutwe kazi, na maafisa wa jeshi wachukue nafasi yao” amesema Kaps Fungaro
Hofu yaenea kwa raia
Hatua ya polisi kukataa kutoa ulinzi kwa wabunge, inatafsiriwa na wachambuzi wa maswala ya usalama na siasa za Uganda akiwemo Charles Rwomushana, kama ya kuogopesha raia wote wa Uganda, na dhihirisho tosha kwamba usalama umedorora kiasi cha walinda usalama kuogopa.
“Hali ya usalama ni mbaya na inaendelea kuzorota kila siku.watoto, wanawake,viongozi wa dini, watu wanauawa kila siku na sasa wabunge wanalengwa. Ukijua kwamba wabunge wamo katika hali ya hatari, mbona wanapewa ulinzi na polisi mmoja ambaye anakaa ndani ya gari moja na mbunge, bila ujasusi wowote?” ameeleza Charles Rwomushana.
Wabunge wataka wahusishwe
wabunge wa upinzani sasa wanataka kuhusiswa kwenye kamati ya usalama ya taifa, lakini Museveni akakataa pendekezo hilo kwamba hawezi kuwaamini wapinzani wake na maswalaya usalama wa nchi.
Museveni pia amesema kwamba aliyekuwa mkuu wa polisi Generali Kale Kayihura, anazuiliwa kutokana na makosa aliyofanya akiwa ofisini, ikiwemo kuwaamini raia Zaidi ya maafisa wake wa polisi katika maswala ya ujasusi na hivyo kufanya maafisa wa polisi kukosa nguvu za kufanya kazi.
Imetayarishwa na mwandishi wetu Kennes Bwire, Washington, DC