Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Desemba 01, 2022 Local time: 20:44

Odinga amlaumu Ruto kwa kupanda kwa gharama ya maisha Kenya na kuendelea kudai kwamba alishinda urais


Kiongozi wa upinzani nchini Kenya Raila Odinga akihutubia waandishi wa habari baada ya kuasilisha kesi mahakamani kupinga matokeo ya kura za urais Agost 22 2022

Mgombea wa urais mara 5 bila mafanikio nchini Kenya Raila Odinga, ameendelea kuishutumu mahakama na tume ya uchaguzi, akidai kwamba alipokonywa ushindi katika uchaguzi mkuu wa mwezi Agosti.

Akihutubia vijana wanaokusanyika kila mara jijini Nairobi, wanaojiita ‘bunge la wananchi’, Raila amesema kwamba “amenyamaza” tangu mahakama ilipomtangaza Dkt William Ruto kuwa mshindi wa uchaguzi mkuu wa mwezi Agosti “lakini hajakubaliana na yaliyotokea”.

‘Mliona ile sarakasi ya mwizi mwingine ambaye vile vile ni mwendawazimu anaitwa Chebukati. Ile tume yake wanne wamesema hapana hii sio kweli, wawili vile vile wamejificha na kubaki pekee yake. Baadaye anasemekana yeye ndiye shujaa. Halafu mahakama ikasema maovu ambayo Chebukati alifanya ndiyo halali,” amesema Odinga, akiongezea kwamba “na mimi nikasema kwamba kama sisi hatutoshi, wakenya wote ambao walijitokeza kupiga kura hawana maana na tukasema tutakaa chini tuone vile tutaendelea”.

Odinga amekuwa akiishutumu kila taasisi ya serikali na jumuiya ya kimataifa, akidai kwamba “walishiriki kumnyima ushindi”.

“Nimekaa kimya sio kwamba nimeridhika. Hapana! Nimekaa kimya kwa sababu nimeona maovu yametendeka. Nahisi vile nyinyi mnahisi.”

Odinga ameilaumu serikali ya Ruto kwa kuendelea kupanda kwa gharama ya maisha

Rais wa Kenya Dkt. William Ruto
Rais wa Kenya Dkt. William Ruto

Amewaambia wafuasi wake kwamba gharama ya maisha nchini Kenya inaendelea kupanda na wakati umefika kuishurutisha serikali kuhakikisha kwamba bei ya bidhaa muhimu inashuka Kenya.

“Najua kwamba bei ya unga imepanda. Bei ya mafuta imepanda. Nauli imepanda. Kodi ya nyumba imepanda. Kila kitu kimepanda na mapato ya wananchi imebaki ile ile. Wakenya wanajisikia vibaya”.

Aliwakumbusha wafuasi wake kuhusu ahadi alizotoa wakati wa kampeni kwamba mpango wake wa kupunguza gharama ya maisha kwa wakenya ulifaa sana kuliko wa serikali iliyopo sasa.

Amekosoa hatua ya serikali ya kuondoa ruzuku ya mafuta na kupelekea bei ya bidhaa hiyo kupanda, akisema ni makosa na ishara ya serikali ya Ruto kutowajali wakenya.

Mwezi mmoja baada ya Rais Ruto kuingia madarakani, Raila amedai kwamba serikali ya Ruto imeshindwa kutekeleza ahadi alizotoa wakati wa kampeni, ikiwemo kutoa pesa kwa vijana kwa ajili ya kuimarisha biashara.

Ruto amekuwa ofisini kama rais kwa muda wa mwezi mmoja pekee

Buneg la Kenya katika kikao Oct 6 2014
Buneg la Kenya katika kikao Oct 6 2014

Baraza la mawaziri la rais William Ruto halijaaidhinishwa na bunge na hivyo Ruto anaendelea kufanya kazi na lililokuwa baraza la mawaziri la rais mstaafu Uhuru Kenyatta.

Hakuna mabadiliko makubwa yametekelezwa serikalini.

Ofisi kadhaa za utekelezaji wa mipango ya rais Ruto, zinasimamiwa na watu walioteuliwa na rais Uhuru Kenyatta.

Bunge limeanza vikao vyake rasmi lakini halijaanza kutekeleza kazi muhimu. Odinga pia amesema serikali ya Ruto imeshindwa kubuni nafasi za kazi kwa vijana.

“Walisema wataweka pesa kwa vijana. Imeonekana? Pesa ya akina mama imeonekana? Ajira imeonekana? Sisi tulisema tutarudisha gharama ya maisha chini. Walikuwa wanamlaumu Uhuru kila mara lakini Uhuru alikuwa anafanya yale ambayo yalikuwa yanafanyika katika ulimwengu mzima”, ameendelea kusema Odinga.

Hata hivyo, ameonekana kulaumu janga la virusi vya Corona kwa kuongezeka kwa gharama ya maisha, akisema kwamba serikali nyingi kote duniani ziliweka ruzuku kwa bidhaa mbalimbali ili kukabiliana na athari za janga la virusi vya Corona.

Amesema vile vile kwamba vita vinavyoendelea Ukraine kutokana na uvamizi wa Russia, vimechangia katika kuongezeka kwa gharama ya maisha kote duniani.

“Uhuru alikuwa anaweka ruzuku kama kinga wananchi wasihangaike. Hawa wamesema kwamba nchi haiwezi kuendelea kuweka ruzuku, wacha wananchi waumie. Wiki hii, bei ya mafuta itapanda tena tuone pale wao watakwenda sasa. Lakini wakenya lazima waangalie mbele. Nina uhakika kwamba wakenya wana uwezo wa kupigana na uongozi wa kimabavu na wataendelea kufanya hivyo ili wajikomboe.”

Siasa za GMO na mbolea ya gharama nafuu

Mkulima wa mahindi, Kwale, Kenya, January 27, 2009.
Mkulima wa mahindi, Kwale, Kenya, January 27, 2009.

Odinga ameendelea kukosoa hatua zote ambazo rais William Ruto amechukua tangu alipoingia madarakani, ikiwemo kuruhusu vyakula vilivyofanyiwa mabadiliko ya kijenetiki maarufu GMO kuanza kukuzwa Kenya.

“Nchi nyingi za Ulaya. Ujerumani, Uholanzi, Italy, Sweden, Austria, Ufaransa zimekataa GMO. Nchi zote ambazo zimeendelea kiuchumi zimekataa GMO kwa sababu wana uhakika kwamba itadhuru maisha ya watu wao. Tunasikia wengine hapa eti wanataka kufanya utafiti. Utafiti gani ambao Kenya itafanya kuliko ule ambao umefanywa na nchi zilizoendela kiuchumi?”

Ameendelea kukosoa hata mipango ya serikali kupunguza bei ya mbolea, akidai kwamba serikali ya Ruto imepewa mbolea kutoka Russia bila malipo yoyote lakini inawauzia wakenya. Amewataka Wakenya kutolipia mbolea hiyo na kwamba waidai serikali iwape bila malipo.

“Hiyo mbolea inakuja wakati wakulima wameshapanda mimea na wanatarajia kuvuna. Wameagiza mbolea ambayo haina kazi. Hawa watu hawana maslahi ya wakenya kwa mipango yao.” Amedai Odinga

Idhaa ya Kiswahili ya Sauti ya Amerika haijaweza kupata ukweli kuhusu madai ya Odinga kwamba Kenya imepewa mbolea na Russia bila malipo.

“Msife moyo, mimi sijakufa moyo. Wakati wa udikteta umekwisha. Siku 40 zinakuja. Siku yao ikifika nyinyi mtaona tu. Si nyinyi mpo hapa? Nipo na subira. Kwa hivyo tutasonga mbele. Mpo tayari?” Odinga amekamilisha hotuba yake kwa wafuasi wake wa bunge mashinani katika bustani ya Jivanjee.

Jumatano mchana, Odinga amewahutubia wafuasi wake katika sehemu tofauti za jiji la Nairobi na kudai kwamba wakati wa kuhakikisha kwamba gaharama ya maisha inarudi chini ni sasa na kwamba hatua za kufanya mabadiliko yanayofaa ni sasa.

Facebook Forum

XS
SM
MD
LG