Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Desemba 07, 2023 Local time: 15:36

Odinga amedai kwamba jumuiya ya kimataifa ilishiriki katika ‘kuiba’ kura Kenya


Kiongozi wa upinzani nchini Kenya Raila Odinga wakati alipofanya maojiano na shirika la habari la Reuters jijini Nairobi. Agosti: 29 2022. PICHA: Reuters
Kiongozi wa upinzani nchini Kenya Raila Odinga wakati alipofanya maojiano na shirika la habari la Reuters jijini Nairobi. Agosti: 29 2022. PICHA: Reuters

Mgombea wa urais mara tano nchini Kenya bila mafanikio Raila Odinga, amedai kwamba alipoteza uchaguzi wa mwezi Agosti mwaka huu kwa sababu nchi za nje ziliingilia uchaguzi huo na kwamba zilimpendelea mpinzani wake.

Bila kutaja mtu wala nchi yoyote, Odinga amesema kwamba wanasiasa wa mirengo ya kulia na makundi yenye pesa kimataifa, yalivuruga uchaguzi wa Kenya.

Katika hotuba ya dakika 22 wakati wa uzinduzi wa kitabu kinachoelezea siasa za Kenya, kilichoandikwa na mkurugenzi mkuu wa chama cha Orange Democratic Movement -- ODM, Oduor Ong’wen, jijini Nairobi, Odinga amedai kwamba matokeo ya uchaguzi wa urais wa Kenya hayakuwa maamuzi ya wakenya.

“Kilichofanyika kilikuwa mapinduzi. Hata mliona mwenyekiti wa tume ya uchaguzi akitangaza matokeo ambayo makamishna wenzake hawakukubaliana nayo na baadaye akatajwa kuwa shujaa, jambo ambalo hawawezi kukubali likafanyika katika nchi nyingine ya Afrika.”

Odinga amesisitiza kwamba “uchaguzi wetu haukuibiwa ndani ya Kenya. Ilikuwa njama za kimataifa.”

“Jumuiya ya kimataifa haikukashifu hatua ya Chebukati (mwenyekiti wa tume ya uchaguzi) kwa sababu walijua kilichokuwa kinaendelea. Wanasiasa wa mirengo ya kulia wamekuwa wakishirikiana na mabwenyenye tangu wakati wa uhuru na wakenya wanastahili kujitolea kwa njia zote ili kushinda nguvu hizo.” Ameendelea kusema Odinga.

Harakati za kukuza demokrasia nchini Kenya

Amekariri kumbukumbu namna wakenya waliopigania demokrasia nchini humo walivyoteseka mikononi mwa utawala wa aliyekuwa rais wa pili hayati Daniel Arap Moi.

Ameeleza namna wanasiasa walivyokamatwa, kuteswa, kupigwa, kuzuiliwa bila kufikishwa mahakamani, na kuuawa kwa kutetea demokrasia na kutaka mabadiliko ya demokrasia nchini Kenya.

“Kuna watu wamesahau haya. Vijana wengi hawajui kilichofanyika nchini humu. Hawajui. Wanajiita ‘hustlers’ kwa sababu hawajui. Kuna hali ya kutojua. Wanatumikia tu utawala ulio madarakani ili kuzima ukweli huu wa kihistoria. Huu ni ukweli ambao unastahili kujulikana. Hatupo hapa kwa sababu ya ukarimu wa watu wengine. Ni kwa sababu watu walihangaika sana ili wakenya wafurahie uhuru ambao upo leo.”

Odinga ameonya kwamba uhuru ambao wakenya wanafurahia sasa, unaweza kutoweka endapo hautalindwa akisisitiza kwamba wakenya wanastahili kusimama imara na kujinyima ili kulinda demokrasia.

“Tunajua kwamba katika harakati hizi lazima tujinyime na wakati mwingine kujinyima kabisa. Wakati mwingine upande wa kushoto unakubaliana na wa kulia. Lakini hiyo haina maana kwamba unasaliti msimamo wako.” Ameendelea kusema Odinga.

Amezungumzia namna alivyolegeza msimamo wake wakati wa utawala wa Daniel Arap Moi, na hata kuhudumu katika serikali, akisema kwamba alitaka kumuonyesha Moi umuhimu wa nchi yenye uhuru na demokrasia.

Mapinduzi ya kijeshi Afrika

Raila Odinga vile vile amesema kwamba nchi za Afrika zinastahili kujikomboa kisisasa na kukuza demokrasia yake.

“Hatutajisalimisha kidemokrasia. Hatutakata tamaa. Mradi wa kukuza demokrasia ya Afrika lazima uendelee. Kutakuwepo changamoto hapa na pale. Tumeanza kuona mapinduzi ya kijeshi yakianza kurudi katika baadhi ya nchi za Afrika. Majenerali wanarudi madarakani na raia wanawakaribisha kwa sherehe na kuwapa maua. Kuna jambo lisilo sahihi lakini hiyo haimaanishi kwamba tukate tamaa.”

Odinga amewahimiza waafrika kulinda raslimali zao na kujiwekea mazingira mazuri ya uhuru na demokrasia.

“Watu wanaoipenda Afrika, wanaotaka mali ya Afrika kutumika vyema, hawajawahi kupata madaraka kulinda na kutumia mali ya waafrika kwa maslahi ya waafrika lakini jumuiya ya kimataifa haitaki kuona Afrika ikiendelea.”

“Ukisema kwamba unataka kuifanya Kenya kuwa nchi yenye viwanda ili bidhaa zake zipatikane katika Afrika Mashariki na Kati, kuna watu wanakosa amani moyoni mwao. Ukisema tusiuze kahawa kabla ya kuitengeneza kwa mfano, hawataki hayo kabisa. Hiyo inaichukiza jumuiya ya kimataifa na ndio sababu hawatutaki tuingie madarakani,” amesema Odinga anayemalizia hotuba yake kwa kuimba wimbo wenye ujumbe kwamba “hata nipigwe teke au nifungwe jela sitarudi nyuma.”

XS
SM
MD
LG