Kama ilivyopangwa, alikutana na mujahedin wanne ambao walikuwa wamekubali kumpeleka kwa kiongozi wao kwa ajili ya mahojiano.
Lakini masaa nne baada ya safari kuanza, Dubois alizibwa macho na kuambiwa iwapo familia yake itashirikiana angeachiliwa. Hapo ndipo alipoelewa kuwa alikuwa ametekwa nyara.
Dubois aliishi takriban miaka miwili akiwa kama mateka kabla ya kufikia hatima ya kuachiliwa tarehe 20 mwezi Machi mwaka 2023, akiwa na mfanyakazi wa Kimarekani wa shirika la misaada Jeffery Woodke.
Katika mahojiano na Sauti ya Amerika, Dubois alizungumza kuhusu yale aliyomkuta, na kushindwa kwake kujaribu kutoroka, na jinsi uandishi wa habari ulivyo mwezesha kujiondoa kutoka kwenye maumivu ya kiakili, kimwili na kihisia.
Kisa cha Dubois inaangazia hatari wanazokabiliana nazo waandishi wa habari wanaofanya kazi katika maeneo yenye migogoro, hususani katika eneo la Sahel lililopo katika barani Afrika, ambako utekaji nyara unaongezeka kwa kasi ya kutisha.
Nchi za Mali, Burkina Faso na Niger zilishuhudia jumla ya matukio ya utekaji nyara 532 katika kipindi cha mwaka 2022, idadi ambayo imeongezeka kutoka matukio 33 mwaka 2017. Kulingana na shirika lisilo la kiserikali la Armed Conflict Location & Event Data Project (ACLED) mpaka sasa inakadiriwa kurekodiwa matukio 158 ya utekaji nyara katika kipindi cha mwaka huu.