Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumapili, Julai 14, 2024 Local time: 13:11

Mwanadiplomasia wa Tanzania Bernard Membe amefariki dunia


Aliyekuwa waziri wa mambo ya nje wa Tanzania Bernard Membe
Aliyekuwa waziri wa mambo ya nje wa Tanzania Bernard Membe

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ametuma ujumbe wa rambi rambi kwa familia na taifa kwa jumla, kufuatia kifo cha aliyekuwa waziri wa mambo ya nje wa Tanzania Benard Membe, aliyefariki dunia asubuhi leo Ijumaawakati akipatiwa matibabu katika hospitali ya Kairuki, mjini Dar-es-salaam.

Membe ambaye alikuwa na umri wa miaka 69 na alikimbizwa hospitali asubuhi ya leo na sababu ya kifo chake haijatangazwa.

Kupitia ukurasa wake wa Twitter, rais Samia amemtaja Membe kuwa mtumishi wa umma aliyefanya kazi yake kwa weledi wa hali ya juu kama mwanadiplomasia, mbunge na waziri aliyeitumikia nchi yake kitaaluma.

Benard Membe alikuwa waziri wa mambo ya nje ya Tanzania kati ya mwaka 2007 na 2015, wakati wa utawala wa rais mstaafu Jakaya Mrisho Kikwete.

Umaarufu wa Membe kisiasa ulianza mwaka 2000 alipochaguliwa kuwa mbunge wa Mtama kupitia chama cha mapinduzi CCM. Alishinda kiti hicho tena mwaka 2005 na 2010.

Benard Membe, ambaye alisomea diplomasia na uhusiano wa kimataifa katika chuo kikuu cha Johns Hopkins, Marekani, alikuwa mtaalam wa maswala ya usalama katika ofisi ya rais kabla ya kuwa mbunge.

Alihudumu katika nafasi mbali mbali nchini Tanzania ikwemo naibu waziri wa nishati na madini lakini alifukuzwa kutoka chama cha CCM mwaka 2020, kwa madai ya kinidhamu na kuvunja kanuni na katiba ya chama kutokana na azma yake kutaka kuwania urais kwa tiketi ya chama cha CCM.

XS
SM
MD
LG