Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Desemba 04, 2023 Local time: 06:00

Muungano wa Ruto umeshinda nafasi zote za spika katika bunge na senate


Moses Wetangula (kulia) akiwa na Kalonzo Musyoka, Isaac Ruto, Raila Odinga na Musalia Mudavadi (kushoto) wakati walipokuwa pamoja katika muungano wa NASA. April 20, 2017. Wetangula amechaguliwa kuwa spika wa bunge la taifa. Musyoka akajiondoa kinyang'anyiro cha spika wa senate
Moses Wetangula (kulia) akiwa na Kalonzo Musyoka, Isaac Ruto, Raila Odinga na Musalia Mudavadi (kushoto) wakati walipokuwa pamoja katika muungano wa NASA. April 20, 2017. Wetangula amechaguliwa kuwa spika wa bunge la taifa. Musyoka akajiondoa kinyang'anyiro cha spika wa senate

Kiongozi wa chama cha Ford Kenya, Moses Wetangula, amechaguliwa kuwa spika wa bunge la taifa la Kenya.

Ford Kenya ni mojawapo ya vyama vinavyounda muungano wa Kenya Kwanza, wa rais mteule William Ruto.

Wetangula, ambaye ni wakili na amekuwa seneta wa Kaunti ya Bungoma kabla ya kujiuzulu na kugombea nafasi ya spika, alikuwa anamuunga mkono Raila Odinga kabla ya wawili hao kukosana na kuvuliwa nafasi ya kiongozi wa walio wachache katika seneti.

Wetangula alikuwa mojawapo ya viongozi waliounda muungano wa NASA, ambao Raila Odinga aliutumia kugombea urais mwaka 2017.

Amepata kura 215 dhidi ya aliyekuwa spika wa bunge hilo la taifa Kenneth Marende, aliyepata kura 130.

Mshindi anastahili kupata kura 233 kati ya 349 lakini Marende amejiondoa katika kinyang’anyiro kabla ya awamu ya pili ya upigaji kura na kukiri kushindwa.

Katika hotuba yake baada ya kuchaguliwa kuwa spika, Wetangula ameahidi “ kuhakikisha kwamba bunge hilo linatekeleza kazi zake vipasavyo kulingana na katiba ya nchi.”

Mwanamke ashinda nafasi ya naibu spika

Mwakilishi wa wanawake wa Kaunti ya Uasin Gishu Gladys Boss Shollei amechaguliwa kuwa naibu wa spika wa bunge la taifa.

Sheli amemshinda Mbunge wa Daddab Farah Maalim. Amepata kura 198 dhidi ya 139.

Maalim amejiondoa katika kinyang’anyiro baada ya duru ya kwanza baada ya mshindi kukosa kupata theluthi mbili ya kura za wabunge wote, sawa na kura 233.

Sholei ni mbunge wa muungano wa Kenya Kwanza, wake rais mteule William Ruto.

Chama cha Raila Odinga kimeshindwa kuwasilisha mgombea wa spika wa Seneti

Katika baraza la seneti, aliyekuwa gavana wa Kilifi Amson Kingi amechaguliwa kuwa spika bila kupingwa.

Hii ni baada ya aliyekuwa makamu rais wa Kenya wakati wa utawala wa Mwai Kibaki, Kalonzo Musyoka kujiondoa kwenye kinyang’anyiro hicho dakika za mwisho na kuacha muungano wa Azimio wake Raila Odinga bila mgombea wa nafasi hiyo.

Kingi amepata kura 46 kati ya 66.

Anakuwa spika wa tatu wa seneti baada ya Ekwe Ethuro na Ken Lusaka. Lusaka alichaguliwa kuwa gavana wa Bungoma.

Maseneta wa muungano wa Azimio, wa Raila Odinga, waliondoka kwenye kikao cha kumchagua spika, baada ya Musyoka kujiondoa.

Wamesusia uchaguzi huo kwa kile walichosema kuwa Amason Kingi anastahili kuchunguzwa kwa kile wanachodai kama ubadhirifu wa fedha wakati alipokuwa gavana wa kaunti ya Kilifi.

Hii ni mara ya kwanza kwa kiongozi kutoka Pwani ya Kenya kuchaguliwa kuwa spika wa baraza la Seneti.

Mgombea wa naibu spika atangazwa mshindi bila mpinzani

Seneta wa kaunti ya Meru Murungi Kathuri naye amechaguliwa kuwa naibu spika wa baraza la seneti bila kupingwa.

Murungi, ambaye pia anatoka muungano wa Kenya Kwanza wa rais mteule William Ruto, alitangazwa kuwa naibu spika baada ya seneta wa Kilifi Steward Madzayo kujiondoa kwenye kinyang’anyiro hicho.

Madzayo alikuwa anagombea nafasi hiyo kwa tiketi ya muungano wa Azimio, wa Raila Odinga.

Spika wa seneti Amason Kingi alitangaza wakati wa hotuba yake kwamba hakuna haja ya kumchagua naibu spika kwa sababu hakuwa na mshindani.

"Ibara ya 11 ya kanuni za bunge zinasema kwamba kama kuna mgombea mmoja wa nafasi ya naibu spika, basi anastahili kutangazwa mshindi.” Amesema Spika Kingi.

Mamlaka ya spika wa bunge la taifa

Kulingana na katiba ya Kenya, spika wa bunge la taifa anashikilia nafasi ya tatu katika uongozi wa nchi, baada ya rais na naibu rais.

Jaji mkuu anashikilia nafasi ya nne.

XS
SM
MD
LG