Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumapili, Julai 14, 2024 Local time: 22:39

Mjadala juu ya kuongezeka ajali za ndege ndogo Kenya


Budget Battle Airport
Budget Battle Airport

Mamlaka ya usalama wa anga nchini Kenya imethibitisha kuwa saa mbili na dakika thelathini na tano Jumapili jioni ndege yenye usajili nambari 5YKDL iliruka kutoka kisiwa cha Ziwa Turkana kuelekea kambi ya watalii ya Lobolo, na muda mfupi tu baadae ilipoteza mawasiliano na kuanguka kisiwani hapo.

Mamlaka hiyo pia inathibitisha kuwa mbali na rubani aliyefariki, watalii raia wa Marekani wanne waliokuwa wamepanda ndege hiyo na kupoteza maisha.

Mabaki ya ndege hiyo aina ya Bell 505 vilitambulika saa tisa usiku na hapakuwepo manusra wowote.

Chini ya kipindi cha wiki tatu, ndege mbili ndogo nchini Kenya zimesababisha maafa ya watu kumi.

Ajali hii ya Jumapili inaibua maswali kadhaa. Eneo linaloripotiwa kuanguka ndege hiyo ni eneo la milima na haifahamiki ni kwa nini ndege hiyo ilikuwa inapaa usiku.

Labda ni mojawapo wa masuala ambayo vyombo vya uchunguzi vitayaweka kwenye mizani kufahamu iwapo palikuwapo na shinikizo au uzembe wa aina yoyote.

Lakini Moses Ndiema, mtaalam wa usafiri wa anga na ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Muungano wa Wafanyakazi wa Mashirika ya Ndege nchini Kenya amedai kuwa utekelezwaji wa sheria hautiliwi maanani.

Aidha, Ndiema anadai kuwa zipo kanuni zinazoongoza usafiri wa angani lakini kufuatana na kumilikiwa kwa ndege hizi na wanasiasa na watu wengine wanaokisiwa kuwa wa vyeo ya juu katika taasisi za serikali, vigezo vinavyotakiwa kufuatwa havifuatwi.

Wiki chache zilizopita ndege nyingine ndogo Cesna 206-5-Y BSE ilipoteza mwelekeo na kuanguka katika msitu wa Makutano eneo la Londiani katika Jimbo la Kericho na kuua watu wengine watano.

Mamlaka ya usafiri wa anga nchini Kenya bado inachunguza visa hivyo. Lakini hali hii inazuwa maswali ya iwapo usafiri wa anga nchini Kenya ni salama kwa ndege ndogo.

Mkasa huu wa ndege ni mojawapo wa mikasa mingi ya ndege ambayo imetukia katika ardhi na anga ya Kenya lakini japo maafisa wa uchunguzi wameeleza kufanya uchunguzi, na hadi hivi sasa uchunguzi huo haujaweka bayana visababishi vya mikasa hiyo.

Pamekuwapo na msururu wa ajali za ndege mara kwa mara nchini Kenya, na matokeo haya yanaibuwa hisia miongoni mwa wadau wa sekta ya usafiri wa anga nchini Kenya.

Februari 13, mwaka huu ndege ndogo ya Flysax 540 Cesna 206-5-Y BSE ilipoteza mwelekeo na kuanguka katika msitu wa Makutano eneo la Londiani katika Jimbo la Kericho na kuwaua watu wengine watano, watatu wakiwa ni raia wa Marekani, rubani mkenya na mtu mwingine mmoja.

Juni 5, mwaka 2018 ndege ndogo kampuni ya ndege ya East Africa Safari Air Express Cesna C208 nambari Y-CAC kutoka Kitale jimbo la Trans-Nzoia magharibi ya Kenya ilipoteza mawasiliano na mtambo wa kudhibiti ndege nchini Kenya. Ndege hiyo ikaanguka katika ukanda wa Aberdares katika jimbo la Nyandarua na kuwaua watu kumi baada ya kutoweka kwa siku kadhaa.

Oktoba mwaka wa 2017, ndege nyingine iliyokuwa imewabeba watu watano ilitumbukia katika Ziwa Nakuru na kuwaua wote waliokuwamo huku vikosi vya uokoaji vikichukuwa wiki kadhaa kuondoa mili katika vifusi vya ndege hiyo.

Juni 10, 2012, mwaka ambao umejijenga katika historia ya Kenya, Waziri wa Usalama wa ndani Prof George Saitoti na waziri msaidizi katika Wizara hiyo Orwa Ojode, walinzi wawili na marubani wawili walipoteza maisha wakati ndege iliokuwa imepaa kutoka uwanja wa ndege wa Wilson ilipoteza mwelekeo na kuanguka katika eneo la Kibiko kwenye Msitu wa Ngong.

Imetayarishwa na Mwandishi wetu, Kennedy Wandera, Kenya

XS
SM
MD
LG