Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatano, Julai 17, 2024 Local time: 19:22

Wadau wa habari waomba muda kujadili kanuni mpya Tanzania


Katibu Mkuu Profesa Elisante Ole Gabriel
Katibu Mkuu Profesa Elisante Ole Gabriel

Mjadala juu ya umuhimu wa kuwa na kanuni nzuri, mifumo na msingi madhubuti ya vyombo vya utangazaji na mitandao ya kijamii Tanzania umepokelewa kwa hisia tofauti na wadau wahabari nchini Tanzania.

Serikali imewasilisha kanuni mpya za maudhui ya vyombo vya utangazaji na mitandao ya kijamii kupitia Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo huku kukiwa na hofu ya uhuru wa habari kudhibitiwa.

Wadau wa habari wamekuwa wakidadisi iwapo kanuni mpya zinaletwa kwa ajili ya kuminya uhuru wa habari na kujieleza au kuboresha tasnia ya utangazaji na mitandao ya kijamii nchini humo..

Kupitia wakili wa mtandao wa kijamii wa Jamii Forums, Benedict Shemakaki amesema kuna baadhi ya vipengele wameviona vinafaa kulingana na muda uliopo, lakini bado kuna vipengele vingine hawavikubali ikiwemo kuwalazimisha kuwatambulisha watoaji wa taarifa za mitandaoni

Wadau hao licha ya kutoa maoni katika baadhi ya vipengele waliomba serikali kuwapatia muda wa wiki moja zaidi ili kupata fursa ya kuzisoma na kuzijadili rasimu za kanuni hizo.

Kanuni hizo mpya zinalengo la kuifanyia maboresho kanuni za Utangazaji za mwaka 2011, huku Kikao cha kwanza cha Kupokea Maoni na Mapendekezo ya wadau kuhusiana na rasimu ya kanuni za maudhui ya Utangazaji na Mitandao ya Kijamii, kikishuhudia serikali ikisisitiza kuwa Maboresho ya kanuni hizo ni kulinda Maslahi ya Taifa.

Profesa Elisante Ole Gabriel Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ameiambia Idhaa ya Kiswahili VOA katika mahojiano maalum kuwa madai hayo ya kudhibiti uhuru wa kujieleza hayana ukweli.

Wizara ya habari utamaduni sanaa na michezo imetoa hadi Oktoba 6 mwaka huu wadau wa vyombo hivyo vya utangazaji na mitandao ya kijamii kuwasilisha kwa maandishi maoni na mapendekezo ya kanuni hizo mpya.

XS
SM
MD
LG