Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumapili, Novemba 27, 2022 Local time: 21:20

McMaster akosoa utumiaji wa kauli ya 'Ugaidi wa Kiislamu' na White House


Rais Donald Trump, kulia, na Luteni Jenerali H R McMaster

Mshauri wa Usalama wa Taifa wa Serikali ya Marekani ameripotiwa kuwaambia wafanyakazi wake kwamba waislamu wanaofanya vitendo vya kigaidi ni waislamu waliopotoka, huo ukiwa ni msimamo tofauti wa itikadi na washauri wengine wa Rais Donald Trump.

Luteni Jenerali H R McMaster, mshauri wa usalama wa taifa, aliwaambia wafanyakazi wa Baraza la Usalama la Taifa kwamba kutumia usemi wa “ugaidi wa Kiislamu” hakuna tija kwa sababu vitendo vya magaidi ni “kinyume cha Uislamu.” Haya ni kwa mujibu wa taarifa ya gazeti la "New York Times."

McMaster aliyatoa maoni hayo siku ya Alhamisi katika mkutano na wafanyakazi wote aliokutana nao kwa mara ya kwanza, kwa mujibu wa waliohudhuria mkutano huo.

Maelezo ya McMaster yanatofautiana na lugha ambayo rais amekuwa akiitumia mara nyingi na yale mtangulizi wake Michael Flynn, ambaye alilazimishwa kujiuzulu baada ya kuwapotosha viongozi kuhusu mawasiliano yake na balozi wa Urusi.

Maoni haya juu ya Uislamu yanaweza kuwa ni dalili za mwanzoni kwamba McMaster anaweza kuliweka mbali baraza hilo na kauli asi za kiitikadi za Flynn.

Wachambuzi wengi wa kisiasa wanasema lugha ya McMaster inalingana zaidi na msimamo wa marais wastaafu Barack Obama na George W. Bush.

Wote wawili walikuwa waangalifu kutenganisha vitendo vya kigaidi mbali kabisa na Uislamu, kwa wasiwasi wao kuwa kwa namna fulani Marekani inahitaji washirika wake katika nchi za Kiislamu kusaidia katika vita dhidi ya ugaidi, na hivyo haingekuwa busara kutumia lugha kama hiyo.

Hata hivyo ushauri wa McMaster katika suala hili la Waislamu unasubiriwa na wengi kuona jinsi atavyoweza kuishawishi White House ambako washauri kadhaa wa rais wanaufahamu tofauti kuhusu Uislam.

Msimamizi wa mikakati katika White House Stephen Bannon, kwa mfano, amekuwa akitahadharisha kukaribia kwa kuzuka kwa vita kati ya Ulimwengu wa Wakiristo na Uislamu.

Facebook Forum

XS
SM
MD
LG