Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Machi 28, 2024 Local time: 15:29

Mbunge wa Chama cha CCM amtembelea Tundu Lissu hospitali Kenya


Lazaro Nyalandu, Mbunge wa Singida Kaskazini (CCM), Tanzania
Lazaro Nyalandu, Mbunge wa Singida Kaskazini (CCM), Tanzania

Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema) nchini Tanzania, Tundu Lissu ambaye amelazwa katika hospitali nchini Nairobi Kenya ameonyesha uso wa tabasamu alipotembelewa na Mbunge wa Singida Kaskazini (CCM) Lazaro Nyalandu.

Nyalandu amesema katika ukurasa wake wa Facebook kuwa Lissu anamshukuru Mungu kwa kumruhusu kuendelea kuwa hai.

“Muda mfupi uliopita, nimeonana na Mh. #TunduLissu katika chumba chake Hospitali ya Nairobi na kuzungumza naye kuhusu hali yake na anavyoendelea.”

“Ukweli ni kwamba, ameumizwa vibaya. Imeelezwa kwamba madaktari wanaendelea na hatua kadhaa za matibabu, wakiwa wameanza kwa kumuimarisha (stabilization), ili kuufanya mwili uweze kumudu hatua zaidi za utibabu anazopaswa kufanyiwa,” amesema Nyalandu.

Amesema anaamini hatua zaidi na za haraka zitahitajika kumsaidia apate huduma za kitabibu katika ubora na ufanisi uliopo kwa sasa duniani.

“Ni maombi yangu kwetu sote, tuweke pembeni tofauti zetu za kiitikadi, ama mitazamo, tuungane na kushikamana kama Taifa kwa ajili ya kumwomba Mungu anyooshe mkono wake na kumponya,” amesema Nyalandu.

Nyalandu amesema, “Sote tuungane kutoa msaada wa hali na mali kwa kadri ya uhitaji wake. Amani iwe naye!”

Lissu anaendelea na matibabu hospitalini hapo baada ya kushambuliwa na kujeruhiwa kwa risasi Septemba 7 akiwa nyumbani kwake Area D mjini Dodoma, Tanzania.

XS
SM
MD
LG