Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Juni 18, 2024 Local time: 14:10

Mazungumzo ya nyuklia yaahirishwa; Marekani yailaumu Iran


Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken

Wanadiplomasia wanaofanya mashauriano huko Vienna kuufufua mkataba wa mwaka 2015 ulioizuia programu ya nyuklia ya Iran wamesitisha mazungumzo mpaka wiki ijayo, wakati maafisa kutoka Marekani na Ulaya wakiikosoa Iran kwa kutopiga hatua.

“Kile tulichokiona katika siku kadhaa zilizopita ni kuwa Iran hivi sasa haionekani kuwa makini kufanya kile kilicho muhimu kurejea kufuata utaratibu, na ndiyo maana tumemaliza duru hii ya mazungumzo Vienna,” Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken alisema Ijumaa, alipohutubia mkutano wa viongozi wa dunia kwa njia ya mtandao uliokuwa umeandaliwa na shirika la habari la Reuters.

“Iwapo njia ya kurejea katika kufuata utaratibu kulingana na mkataba haitawezekana, tutatafuta njia nyingine mbadala,” alisema, bila ya kutoa ufafanuzi zaidi.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Marekani alisema Ijumaa ikiwa ni taarifa ya zamani kuwa duru za mazungumzo ya awali na Iran “zilikuwa zimepiga hatua, kupata muafaka kwa masuluhisho mbalimbali kwenye masuala magumu sana ambayo yalikuwa na utata kwa pande zote.” Lakini, alisema, “Mwenendo wa Iran wiki hii bahati mbaya, haukuwa wa kujaribu kutatua masuala yaliyokuwa yamebakia.”

Maafisa wa Ulaya pia wameelezea kukerwa na Iran kuhusu mazungumzo, yaliokuwa yameanza Jumatatu.

Mwakilishi wa Umoja wa Ulaya katika mazungumzo ya nyuklia ya Iran Enrique Mora na kiongozi wa mazungumzo ya nyuklia kwa upande wa Iran Ali Bagheri Kani wakisubiri kuanza mkutano Vienna, Austria Novemba 29, 2021. REUETRS
Mwakilishi wa Umoja wa Ulaya katika mazungumzo ya nyuklia ya Iran Enrique Mora na kiongozi wa mazungumzo ya nyuklia kwa upande wa Iran Ali Bagheri Kani wakisubiri kuanza mkutano Vienna, Austria Novemba 29, 2021. REUETRS


Taarifa ya Ijumaa kutoka kwa maafisa wa ngazi ya juu wa Ufaransa, Uingereza na Ujerumani – mataifa matatu ya Ulaya yenye nguvu yanayoshiriki kama wapatanishi katika mazungumzo ya nyuklia – wamesema, “Wiki hii [Iran] imerudisha nyuma mafanikio ya kidiplomasia yaliyokuwa yamefikiwa.”

Marekani na Iran walianza tena mashauriano yasiokuwa ya moja kwa moja huko Vienna Jumatatu, huku wapatanishi wakitafuta kuzileta pande zote mbili kutekeleza makubaliano ya mwaka 2015, yanayojulikana kama Mpango wa Hatua Kamili ya Pamoja, au JCPOA.

Wapatanishi wa Marekani na Iran walikutana siku za nyuma katika mazungumzo yasiokuwa ya moja kwa moja bila ya kufikia hitimisho mara sita tangu Aprili mpaka Juni, wakati Iran ilipositisha mazungumzo kabla ya uchaguzi wa rais.

Chini ya mpango wa JCPOA, Iran iliahidi itasitisha harakati za nyuklia ambazo zingeweza kupelekea utengenezaji wa silaha kwa mabadlishano ya ahueni ya vikwazo vya kimataifa. Tehran inakanusha inataka kutengeneza silaha za nyuklia.

Utawala uliotangulia wa Marekani wa Rais wa zamani Donald Trump ulijiondoa katika makubaliano ya JCPOA mwaka 2018, ukisema ulikuwa siyo imara dhidi ya Iran, na ukarejesha vikwazo vya Marekani.

Iran ilijibu mwaka mmoja baadae kwa kuanza hadharani kuvuka viwango vya makbaliano ya JCPOA katika shughuli zake za nyuklia. Mrithi wa Trump, Rais Joe Biden, amesema anataka kuendeleza makubaliano tena iwapo Iran itafanya hivyo.

Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomic limethibitisha ukiukaji wa karibuni wa viwango vya makubaliano ya JCPOA Jumatano, wakisema wameanza uzalishaji wa hatua ya juu katika kinu chake cha nyuklia huko Fordo kwa kusindika uranium kufikia asilimia 20 ya uasilia, ikiwa ni hatua chache to kufikia viwango vya utengenezaji silaha.

Israel, ambaye ni mshirika mkuu wa Marekani ambaye Iran imeapa kuiangamiza, imeshtushwa na habari hizo za kiwango cha usindikaji wa uranium.

Serikali ya Israeli imesema Waziri Mkuu Naftali Bennett alizungumza kwa simu na Blinken Alhamisi, aliishutumu Tehran kutumia mafanikio ya kituo cha nyuklia ya Fordo kama “usaliti wa kinyuklia” dhidi ya mazungumzo ya JCPOA.

Israeli imesema Bennett aliitaka Marekani na nchi nyingine zenye nguvu kuchukua hatua kwa kusimamisha mazungumzo hayo mara moja.

Vyanzo vya habari hii ni VOA, Mashirika ya Habari ya AFP na Reuters

XS
SM
MD
LG