Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Aprili 16, 2024 Local time: 13:50

Mwanaharakati ataka mkutano wa Makka uchukue hatua kali dhidi ya Myanmar


Maandamano makubwa yanaendelea duniani kulaani mauaji ya kinyama yanayofanywa na majeshi ya Myanmar dhidi ya waislam wa kabila dogo la Rohingya.

Guterres: Ghasia lazima zisitishwe Myanmar
please wait

No media source currently available

0:00 0:06:00 0:00

Pia serikali mbalimbali ulimwenguni zimeendelea kupaza sauti dhidi ya vitendo vya kuuawa watu hao lakini duru za habari zimeripoti kuwa pamoja na kutolewa onyo kali ukatili huo umeendelea kuwakabili Waislam katika nchi hiyo ambao wamekuwa wakikimbia mashambulizi hayo.

Mwanaharakati wa kisiasa wa kabila hilo la Rohingya Mohamed Noor amekaririwa na kituo cha Televisheni cha Al-Jazeera akisema kuwa "lazima hatua za kisheria zichukuliwe dhidi ya utawala wa Myanmar… Nasisitiza mkutano mkuu wa Mecca, Saudi Arabia lazima uchukue hatua kali na chanya dhidi ya Myanmar."

“Ni kusudio la serikali ya Myanmar kulazimisha kuwafukuza watu wa kabila la Rohingya kutoka katika ardhi ya mababu zao… lakini ili kupata ufumbuzi juu ya suala hili ni lazima tulete demokrasia nchini Myanmar… kwa sababu Myanmar sio demokrasia bali ni utawala wa mabavu wa kijeshi unaoweza kuamua kufanya kitu chochote, amesema mwenyekiti mwenza wa baraza la mawakili la Bangabandhu, Uingereza,” Al Jazeera imeripoti.

Lakini kiongozi wa wengi katika bunge la senate nchini Marekani, Mitch McConnell, amesema kuwa kiongozi wa Burma Aung San Suu Kyi amekubali kuwaruhusu zaidi maafisa wa kutoa msaada kwa Waislamu wa kabila dogo la Rohingya na amechukuwa jukumu la kuhakikisha hilo linafanyika.

Kiongozi huyo pia amesema ukiukaji wa haki za binadamu utahitaji kushughulikiwa lakini akasisitiza kuwa hana uwezo wa kuliamuru jeshi la taifa hilo lenye ushawishi mkubwa.

Awali waziri wa mashauri ya nchi za kigeni wa marekani, Rex Tillerson, alisema kuwa serikali ya Myanmar ni sharti ikome kuwanyanyasa Waislamu wa kabila la Rohingya.

Kiongozi wa Myanmar anakabiliwa na lawama za kushindwa kulisimamia swala la machafuko huko Myanmar.

Machafuko hayo yamelazimisha Waislamu wa kabila la Rohingya takriban 370,000 kukimbilia kuvuka mpaka wa Bangladesh.

Aung San Suu Kyi, amekuwa taswira ya demokrasia kutokana na kushikiliwa kwake kwa kipindi kirefu na utawala wa zamani wa Myanmar wa kijeshi.

Lakini msimamo wake tofauti dhidi ya matatizo yanayowakabili Waislam wa Rohingya katika jimbo la Rakhine- akikanusha kuwa habari nyingi juu ya tatizo hilo ni “taarifa za uongo” ambazo zinalengo la kusaidia maslahi ya “magaidi”.

Kauli yake hiyo imemsababishia kupoteza heshima yake kwa serikali mbalimbali na wanaharakati wa haki za kibinadamu ulimwenguni, wakiwemo baadhi ya wale waliowahi kutunukiwa tuzo ya amani ya Nobel kama yake.

Vyanzo vya habari nchini Myanmar vinaeleza kuwa Waislam wa nchi hiyo wamekuwa wakikimbia kuelekea India na Bangladesh.

Kwa mujibu wa ripoti ya Umoja wa Mataifa, helikopta za kijeshi zimeendelea kupiga risasi maeneo ya Waislam.

Ripoti hiyo pia inasema kuwa kwa miaka 10 iliyopita, Jeshi la nchi hiyo limekuwa likiwatafuta watu wazima wa jamii hiyo ya Waislam na kuwaua na ndiyo sababu watu wa Rohingya wanakimbilia Bangladesh. Hata hivyo serikali ya Myanmar imekanusha tuhuma hizo dhidi ya Jeshi lake.

XS
SM
MD
LG