Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Julai 22, 2024 Local time: 08:37

Matukio muhimu Afrika 2022


Mkutano wa viongozi wa nchi za Afrika katika makao makuu ya Umoja wa Afrika, Addis Ababa, Ethiopia, Feb. 5, 2022.
Mkutano wa viongozi wa nchi za Afrika katika makao makuu ya Umoja wa Afrika, Addis Ababa, Ethiopia, Feb. 5, 2022.

Matukio mengi Afrika mwaka 2022 yamezunguka sana Afrika magharibi kutokana na ukosefu wa usalama na mapinduzi ya kijeshi.

Vyombo vya habari viliangazia pia vita vya waasi katika Jamhuri ya kidemokraia ya Congo kutokana na shutuma kwamba nchi Jirani zinahusika na mgogoro huo huku kwa mara ya kwanza, jumuiya ya Afrika ya mashariki ikiweka mikakati ya kusuluhisha mgogoro wa DRC.

Kusini mwa Afrika, majanga yaliripotiwa zaidi, huku nchi za Afrika zilizo kwenye muungano wa nchi za kiarabu zikikutana lakini bila kufikia makubaliano.

Matokeo ya uchaguzi katika nchi zote zilizoandaa zoezi hilo yalikataliwa na upinzani kwa sababu tofauti.

Mwaka 2022 umekuwa wenye masumbuko mengi kwa nchi kadhaa za Afrika hasa kutokana na kuongezeka kwa gharama ya Maisha na ukuaji wa uchumi kushuka kwa kiwangokikubwa baada ya janga la virusi vya Corona na hatimaye Russia kuvamia Ukraine kivita na kupelekea ukosefu wa nafaka, ngano, mafuta ya kupika na kupatanda kwa bei ya mafuta.

Nchi za Afrika, tayari zikiwa na matatizo yake ya ndani, ziliathirika pakubwa, lakini pia juhudi za kidiplomasia zilichukuliwa na mataifa ya Afrika kujiondoa kwenye matatizo.

Katibu mkuu wa jumuiya ya nchi za kiarabu Ahmed Aboul Gheit akizungumza wakati wa mkutano wa nchi za kiarabu mjini Algiers, Algeria. Nov. 2, 2022.
Katibu mkuu wa jumuiya ya nchi za kiarabu Ahmed Aboul Gheit akizungumza wakati wa mkutano wa nchi za kiarabu mjini Algiers, Algeria. Nov. 2, 2022.

Mkutano wa nchi za kiarabu Algeria

Algeria ilikuwa mwenyeji wa kongamano la nchi za kiarabu lakini baadhi ya viongozi hawakuhudhuria, ikiwa ni ishara za mpasuko katika ulimwengu wa kiarabu.

Algeria ni nchi kubwa ya kiarabu barani Afrika na imekosoa sana makubaliano maarufu ya Abraham, na ilivunja uhusiano wa karibu kati ya Morocco na Isreal, baada ya Israel kufungua ubalozi wake mjini Rabat.

Algeria ina uhusiano mwema na Palestina. Algria vile vile inaunga mkono uhuru wa Western Sahara inayotawaliwa na Morocco.

Rais wa Algeria Abdelmadjid Tebboune alikuwa mwenyekiti wa kongamano hilo, lililohudhuriwa na rais wa Misri Abdul Fattah Sisi, pamoja na marais wa Tunisia, Iraqi, Somali na Palestina.

Viongozi wengine walikuwa kiongozi wa umoja wa falme za kiarabu, Qatar na Sultan wa Oman.

Mwana wa ufalme wa Saudi Arabia Mohammed bin Salman na mfalme Salman, hawakuhudhuria, saw ana mfalme wa Morocco Mohammed VI, mfalme wa Bahrain na Amir wa Kuwait.

Miongoni mwa yaliyojadiliwa ni namna ya kusuluhisha mgogoro kati ya nchi za kiarabu na Israel.

Karatasi la kupiga kura nchini Angola. picha ilipigwa katika kituo cha kupigia kura cha Ninga Mbandi, mji mkuu wa Luanda, Angola. Aug 24, 2022
Karatasi la kupiga kura nchini Angola. picha ilipigwa katika kituo cha kupigia kura cha Ninga Mbandi, mji mkuu wa Luanda, Angola. Aug 24, 2022

Uchaguzi mkuu Angola

Uchaguzi mkuu wa Angola uliofanyika mwezi Agosti uliishia mahakamani baada ya majaji katika mahakama ya kikatiba kutupilia mbali kesi ya kupinga ushindi uliompa mhula wa pili mdarakani rais Joao Lourenco na chama chake cha Movement for liberation of Angola MPLA.

Tume ya uchaguzi ilitangaza ushindi wa Lourencio na kuendeleza miongo mitano ya utawala wa chama cha MPLA, bada ya chama hicho kupata ushindi wa asilimia 51.

Chama cha National union for the total independence of Angola UNITA, kikiongozwa na Adalberto Costa Junior, kilipinga matokeo hayo yaliyokipatia asilimia 44 ya kura zote zilizopigwa. Costa Junior alidai kwamba kulikuwa na wizi mkubwa wa kura na kushutumu tume ya uchaguzi ambayo inaongzwa na watu waliochaguliwa na chama cha MPLA kwa udanganyifu huo, ikiwemo madai ya wafu kupiga kura.

UNITA kilidai kwamba hakuna msindi alikuwa amepatikana katika duru ya kwanza ya uchaguzi, madai ambayo yaliungwa mkono na shirika la kiraia la Mudei.

Uamuzi wa mahakama ya kikatiba ulikuwa wa mwisho na haungeweza kupingwa mahali popote, na hivyo kufungua njia kwa Lourenco kuapishwa.

Rais wa Kenya Dr. William Ruto aliyechaguliwa katika uchaguzi wa mwezi Agosti uliokuwa na ushindani mkali. Alimshinda mwanasiasa wa muda mrefu Raila Odinga
Rais wa Kenya Dr. William Ruto aliyechaguliwa katika uchaguzi wa mwezi Agosti uliokuwa na ushindani mkali. Alimshinda mwanasiasa wa muda mrefu Raila Odinga

Uchaguzi mkuu wa Kenya

Utata kuhusiana na matokeo ya uchaguzi pia ulitokea nchini Kenya. Mwanasiasa wa upinzani wa muda mrefu Raila Odinga alipinga matokeo ya uchaguzi yaliyomtangaza Dr. William Ruto kuwa mshindi wa uchaguzi huo.

Tofauti na Angola, tume ya uchaguzi ya Kenya iligawanyika dakika za mwisho kabla ya mwenyekiti wake Wafula Chebukati kutangaza matokeo rasmi.

Ruto, alimshinda Odinga baada ya kupata asilimia 50.5 ya kura zilizopigwa.

Makamishna wanne wa tume ya uchaguzi wakiongozwa na naibu mwenyekiti Juliana Cherera, walijitenga na matokeo yaliyotangazwa wakidai kwamba yalikuwa yanajumulishwa kwa njia ya siri.

Odinga aliasilisha kesi mahakamani, na baadaye kesi hiyo kutupiliwa mbali na majaji woet wote wakisema kesi haikuwa na ushahidi wowote.

Kinachoendelea sasa ni makamishan waliopinga matokeo kuchunguzwa kutokana na madai kwamba walikuwa wakishirikiana na maafisa serikalini na katika muungano wa Raila Odinga kuhujumu uchaguzi huo.

Baadhi ya makamishna wamejiuzulu, na ushahidi dhidi yao umeanza kutolewa.

Mwanachama wa chama cha African national congress akiwa amesisimama karibu na picha inayoonyesha nembo ya chama hicho wakati wa kongamano la 55 la chana, mjini Johannesburg, Afrika kusini, Dec. 18, 2022.
Mwanachama wa chama cha African national congress akiwa amesisimama karibu na picha inayoonyesha nembo ya chama hicho wakati wa kongamano la 55 la chana, mjini Johannesburg, Afrika kusini, Dec. 18, 2022.

Siasa za Afrika kusini, Ramaphosa anusurika kura ya kutokuwa na Imani naye

Rais wa Afrika kusini Cyril Ramaphosa, alichaguliwa kuwa mwenyekiti wa chama kinachotawala cha African national Congress ANC baada ya kunusurika kura ya kutokuwa na Imani naye bungeni.

Ramaphosa anaandamana na kashfa ya utakatishaji wa pesa. Ripoti ya kwanza kutaka achunguzwe zaidi iliimwa na bunge lenye wabunge wengi wa chama anachoongoza.

Katika uchaguzi wa chama, alikuwa anakabiliwa na upinzani kutoka kwa aliyekuwa waziri wake wa afya Zweli Mkhize, ambaye vile vile alitimuliwa kutoka baraza la mawaziri kutokana na sakata ufisadi, na wote wamekana kabisa madai yanayowaandaman.

Kuchaguliwa kwa Ramaphosa ni tabasamu ya muda kwake na wafuasi wake, kwa sababu bado anachunguzwa na polisi, ofisi ya ushuru na benki kuu kuhusiana na madai ya utakatishaji wa pesa, baada ya kuibwa kwa dola 580,000 zilizokuwa zimefichwa kwa kiti shambani mwake, na akakosa kuripoti wizi huo kwa mamlaka husika.

Kamati ya wataalam wa sheria iliyoteuliwa na spika wa bunge, ilisema katika ripoti yake kwamba Ramaphosa ana kesi ya kujibu, na kwamba huenda alivunja sheria za kupambana na ufisadi na katiba.

Lakini bunge lilitupilia mbali ripoti hiyo na kumsafisha Ramaphosa. Amekanusha kabisa kufanya kosa lolote.

Ushindi huo unamueka katika nafasi nzuri ya kugombea mhula wa pili wa urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2024.

Matukio ya mapinduzi ya serikali yaliyoanza mwaka 2020 katika nchi za Afrika magharibi, bado yameendelea mwaka huu 2022.

Kiongozi wa mapinduzi ya kijeshi nchini Burkina Faso Ibrahim Traore
Kiongozi wa mapinduzi ya kijeshi nchini Burkina Faso Ibrahim Traore

Mapinduzi ya kijeshi Burkina Faso, Mali, Guinea Bissau, Gambia

Septemba 30, wanajeshi walimpindua rais wa Burkina Faso walimpindua kiongozi wa muda Paul Henri Sandaogo Damiba wakidai kwamba alikuwa ameshindwa kukabiliana na ukosefu wa usalama nchini humo kutokana na mashambulizi ya kila mara ya makundi ya kiislamu.

Damiba alikuwa amekaa madarakani kwa muda wa miezi 8 baada ya kupindua serikali ya Roch Marc Christian Kabore aliyetawala nchi hiyo kwa miaka 6.

Burkina Faso sasa inaongozwa na Capteni Ibrahim Traore mwenye umri wa miaka 34, baada ya mapinduzi hayo juu ya mapinduzi.

Jaribio la mapinduzi lilizimwa nchini Mali.

Serikali ambayo iliingia madarakani Agosti mwaka 2020 baada ya kutekeleza mapinduzi ilidai kwamba kulikuwa na njama za nchi za magharibi kuipindua.

Jaribio la mapinduzi lilifeli nchini Guinea Bissau kumuondoa rais Umaru Sissoco Embalo, sawa na nchini Gambia ambapo wanajeshi wanne waliripotiwa kukamatwa na wengine kadhaa kuchunguzwa baada ya kujaribu kupindua utawala wa rais Adama Barrow, huku umoja wa Afrika na jumuiya ya kiuchumi ya Afrika magharibi ECOWAS wakishutumu tukio hilo.

Makubaliano ya amani kati ya serikali ya Senegal na waasi

Nchini Senegal, serikali ilifikia makubaliano na kundi la waasi la Cesamance na kumaliza mgogoro wa muda mrefu zaidi Afrika ulioanza mwaka 1982.

Makubaliano hayo pia yalihusisha makundi ya waasi ya Chad baada ya mazungumzo yaliyofanyika mjini Doha kwa usimamizi wa Qatar.

Makubaliano hayo yalipatikana baada ya kifo cha aliyekuwa rais wa Chad Idris Derby mwaka uliopita 2021, aliyefariki akiwa katika msitari wa mbele wa mapigano na makundi ya waasi.

Rais wa DRC Felix Tshisekedi na mwenzake wa Rwanda Paul Kagame
Rais wa DRC Felix Tshisekedi na mwenzake wa Rwanda Paul Kagame

Mapigano ya waasi Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo

Mwaka huu wa 2022, mapigano yameendelea mashariki mwa Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, makundi ya waasi yakipigana na wanajeshi wa serikali huku raia wakiuawa na maelfu kukoseshwa makao.

Kundi la Waasi la M23 limesababisha mgogoro wa kidiplomasia kati ya DRC na Rwanda, huku Uganda nayo ikitajwa kwenye mgogoro huo.

DRC imeituhumu Rwanda kwa kuunga mkono waasi hao na kuwapa silaha.

Mara kadhaa, Rwanda imekana madai hayo, lakini imepokea shinkizo kutoka kwa Marekani, Ufaransa, Ujerumani, Ubelgiji miongoni mwa nchi nyingine pamoja na mashirika ya kuetetea haki za kibinadamu, kuacha kuunga mkono waasi hao.

Majibizano makali yalitokea kati ya rais wa DRC Felix Tshisekedi na rais wa Rwanda Paul Kagame kuhusu vita mashariki mwa DRC, huku raia wa DRC wakiandamana hadi kwenye mpaka wa DRC na Rwanda. Ripoti kadhaa ikiwemo ya umoja wa mataifa zimehusisha Rwanda na waasi wa M23.

Juhudi za kidiplomasia zikiongozwa na aliyekuwa rais wa Kenya Uhuru Kenyatta, pamoja na rais wa Angola, zilifanikiwa kuwakusanya viongozi wa makundi kadhaa ya waasi mjini Nairobi kenya na kukubaliana kuacha mapigano.

Jumuiya ya Afrika mashariki ilituma wanajeshi mashariki mwa DRC, wakiongozwa na kamanda wa kutoka Kenya Generali Jeff Nyaga. Waasi wa M23 walikubali kuondoka sehemu walizokuwa wameshikilia.

Aliyekuwa rais wa Kenya Uhuru Kenyatta akiwashukuru mwakilishi wa serikali kuu ya Ethiopia Redwan Hussein na mwakilishi wa Tigray Getachew Reda, baada ya kusaini mkataba wa amani Ethiopia, Pretoria, Afrika kusini, Novemba 2, 2022
Aliyekuwa rais wa Kenya Uhuru Kenyatta akiwashukuru mwakilishi wa serikali kuu ya Ethiopia Redwan Hussein na mwakilishi wa Tigray Getachew Reda, baada ya kusaini mkataba wa amani Ethiopia, Pretoria, Afrika kusini, Novemba 2, 2022

Makubaliano ya amani Ethiopia

Diplomasia ilifanikiwa katika kusitisha vita vya Ethiopia kati ya wanajeshi wa serikali na wapiganaji wa Tigray.

Pande zinazohasimiana zilikubaliana kusitisha vita kabisa baada ya mapigano ya miaka miwili, katika mazungumzo yaliyofanyika Afrika kusini.

Mapigano hayo yalisababisha vifo vya maelfu ya watu.

Mazungumzo yaliongozwa na mjumbe wa umoja wa Afrika Olusegun Obasanjo.

Mfumuko wa bei Nigeria, Sierra Leone, Senegal na Ghana

Mfumuko wa bei ulipanda na kufika asilimia 21.47 nchini Nigeria, kiwango ambacho hakijawahi kutokea kwa muda wa miaka 17.

Asilimia 63 ya watu wote Nigeria waliripotiwa kuwa maskini katika nchi hiyo mzalishaji mkubwa wa mafuta, kubwa zaidi Afrika na yenye idadi kubwa ya watu.

Waandamanaji walijitokeza barabarani kulalamikia hali ngumu ya Maisha nchini Sierra Leone na kutaka rais Julius Bio kujiuzulu wakisema ameshindwa kujenga uchumi wa nchi hiyo.

Maandamano hayo yalipelekea vifo vya watu 21 na maafisa wa polisi sita.

Gharama ya juu ya Maisha ilipelekea Serikali ya Senegal kutangaza ruzuku ya dola milioni 762 ili kukabiliana na kuongezeka kwa bei ya vitu muhimu.

Ghana ililazimika kukopa dola bilioni 3 kutoka shirika la fedha ulimwenguni IMF, baada ya sarafu ya ghana kuanguka kabisa kwa thamani dhidi yad ola, huku mfumuko wa bei ukifikia asilimia 40.

Wanajeshi wa Burkina Faso wakipiga doria
Wanajeshi wa Burkina Faso wakipiga doria

Kuongezeka kwa makundi yenye silaha Sahel

Makundi yenye silaha yameongezeka nchini Mali ambayo uhusiano wake na Ufaransa uliharibika zaidi mwaka huu kiasi cha Ufaransa kujiondoa Mali katika ushirikiano wa kulinda usalama katika kanda ya Sahel.

Utawala wa kijeshi wa Mali uliwakamata na kuwazuia wanajeshi 48 wa Ivory coast na kuharibu uhusiano kati ya nchi hizo mbili kiasi cha Ivory Coast kuondoa wanajeshi wake kutoka kikosi cha kulinda amani cha umoja wa mataifa.

Maandamano yalitokea mjini Bamako kukashifu Ufaransa huku yakisifu Russia. Utawala wa Mali unashirikiana na kundi la mamluki kutoka Russia la Wagner kukabiliana na makundi ya wapiganaji nchini humo.

Nchi 35 za Afrika hazikushiriki katika kura ya kuiwajibisha Russia kutokana na uvamizi wake nchini Ukraine, ikiwa ni mojawapo ya dalili za Russia kuimarisha uwepo wake Afrika.

Wanajeshi wa Ufaransa wameondoka Mali na kuingia Niger ambayo sasa ndio kambi yake ya kusaidia kiusalama eneo la Sahel.

Rais Samia suluhu Hassan akihutubia taifa baada ya kula kiapo
Rais Samia suluhu Hassan akihutubia taifa baada ya kula kiapo

Mjadala kuhusu denial serikali Tanzania

Nchini Tanzania mwaka huu umekuwa wa mjdala mkubwa kuhusu kuongezeka kwa deni la taifa na kufikia Trilioni 91 huku serikali ikiendelea kukopa.

Rais Samia Suluhu Hassan, amekosolewa sana kwa kukopa, kiasi cha kutokea mvutano ndani ya chama cha mapinduzi CCM, kinachotawala Tanzania.

Aliyekuwa Spika Job Ndugai alilazimika kujiuzulu baada ya kukosoa hadharani utawala wa rais Suluhu Hassan, akisema kwamba nchi ilikuwa inapigwa mnada kwa kuongeza kukopa kila mara.

Mjadala mkubwa Tanzania ni kwamba nchi inakopa lakini mabadiliko ya kiuchumi katika Maisha ya raia wa Tanzania hayaoenikani.

Siasa kuelekea mwaka 2023

Tunapoingia mwaka 2023, nchi kadhaa za Afrika zinajitayarisha kwa uchaguzi mkuu. Muda wa kuwa madarakani wa Felix Tshisekedi wa Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo unamalizika na inabidi atafute tena idhini ya wapiga kura.

Ushindani mkali unatarajiwa katika nchi hiyo ya pili kwa ukubwa Afrika na yenye utajiri mkubwa wa madini lakini raia wake wengi ni maskini na wanakabiliwa na ukosefu wa usalama.

Kampeni zinaendelea Nigeria, maswala kuu yakiwa uchumi na usalama. Rais Muhamadu Buhari anamaliza mhula wake wa pili madarakani mwezi May.

Kuna ishara kwamba huenda rais Macky Sall wa Senegal akatangaza kugombea mhula wa tatu madarakani katika uchaguzi wa mwaka ujao.

Julius Maada Bio wa Sierra Leone na George Weah wa Liberia pia watagombea urais kwa mara nyingine katika uchaguzi wa mwaka ujao.

XS
SM
MD
LG