Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Machi 29, 2024 Local time: 13:22

Marekani yataka Zimbabwe itekeleze ahadi ndipo vikwazo viondolewe


Balozi Brian Nichols
Balozi Brian Nichols

Balozi mpya wa Marekani nchini Zimbabwe, Brian Nichols, amesema kuwa Zimbabwe lazima itekeleze ahadi ya mageuzi iliyotangaza iwapo inataka vikwazo ilivyowekewa na Marekani viondolewe.

Katika mahojiano Ijumaa na VOA katika jengo la makao makuu ya Sauti ya Amerika, Washington, DC, Balozi Nichols amesema kuwa serikali mpya iliochaguliwa Zimbabwe ya Rais Emmerson Mnangagwa itapata kuungwa mkono kikamilifu na serikali ya Marekani ikiwa itatekeleza mabadiliko ya kisheria iliyo ahidi wakati wa kampeni za uchaguzi.

Amesema mageuzi hayo ni pamoja na kufuata utawala wa sheria na kuruhusu wananchi uhuru wao wa kupasha habari na uhuru wakueleza wanachotaka.

Vikwazo vyarudishwa upya

Mwezi uliopita, Rais wa Marekani Donald Trump alirudisha vikwazo upya dhidi ya Zimbabwe na kuweka utaratibu ambao nchi inatakiwa kufuata ili vikwazo hivyo viondoshwe.

Sheria ya urais, iliyoitwa Marekebisho ya Sheria ya 2018 ya Demokrasia na Kufufua Uchumi Zimbabwe, ambayo pia inajulikana kama Zidera, ilikuwa imeweka sharti moja la kuhakikisha uchaguzi mkuu Julai ulikuwa huru na haki.

Kufuatia chaguzi hizo, chama tawala ZANU-PF kilitangazwa mshindi, lakini upinzani ulipinga matokeo hayo ukidai kulikuwa na wizi. Mahakama ya Katiba ilisikiliza kesi juu ya mvutano huo Agosti 2018, ikitoa uamuzi dhidi ya madai ya upinzani kwamba uchaguzi ulikuwa umechakachuliwa.

Uchaguzi huo, ambao wengi walisema ulikuwa wa amani ukilinganisha na miaka iliyopita, hata hivyo haukusalimika kutokana na vurugu zote. Jeshi la nchi hiyo liliripotiwa kutumia risasi za moto na kuwauwa watu wasiopungua sita wakati wa maandamano yaliyofanywa na upinzani kupinga juu ya utaratibu wa upigaji kura.

Balozi Nichols amesema tayari ameshakutana na pande zote, Rais Mnangagwa na kiongozi wa upinzani Nelson Chamisa na anatarajia kushirikiana na wote katika kutekeleza majukumu yake.

“Nafikiri wote wawili ni watu wenye kuipenda nchi yao, na wanania ya kuleta mabadiliko na kutatua matatizo mengi yaliyokuwepo zamani,” amesema.

XS
SM
MD
LG