Wizara ya mambo ya nje ya Marekani imetangaza vikwazo hivyo dhidi ya makundi mawili yanayohusishwa na kikosi maalum cha ulinzi cha Iran, kwa kusema walihusika katika utafiti na utengenezaji wa makombora ya masafa marefu.
Imeendelea kusema kwamba harakati za Iran katika Mashariki ya Kati zinahatarisha uthabiti, usalama na ustawi wa kieneo.
Wakati huo huo, wizara ya fedha ya Marekani imewawekea vikwazo watu watano na taasisi saba kwa kuunga mkono manunuzi ya jeshi la Iran pamoja na raia watatu wengine wa Iran kwa kusema ni sehemu ya kundi la kihalifu lenye makao yake Iran.
Vikwazo hivyo vitazuilia rasilmali za hao Wairan wanaokusudiwa iwapo zinaweza kuwepo Marekani na kuwazuia Wamarekani wasifanye biashara yoyote na watu hao.
Huko Umoja wa Mataifa New York, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Mohammad Zarif ameiambia VOA kuwa vikwazo “kwa masikitiko makubwa vimekuwa ni tabia mbaya” kwa upande wa Marekani, na kwa hivyo Marekani itegemee kuwa Iran italipiza kisasi.
“itawahusisha watu ambao wameshiriki katika ugaidi na siasa kali katika eneo la Mashariki ya Kati pia wale wanaosaidia uvamizi wa ardhi zetu,” Zarif amesema.
Ameongeza kuwa tangazo juu ya kulipiza kisasi dhidi ya vikwazo vya Marekani vitafuatia muda hivi karibuni.