Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumapili, Oktoba 01, 2023 Local time: 12:51

Marekani yaanza kutoa msaada wa dharura Lebanon


Waziri wa Mambo ya Nje Michael Pompeo

Marekani inapeleka misaada ya dharura Lebanon, ikianza kutuma chakula, maji na mahitaji ya tiba, chini ya maelekezo ya Rais Donald J.Trump kufuatia mlipuko wa Jumanne mjini Beirut, mshauri wa usalama wa taifa Robert C. O’Brien amesema Ijumaa.

Hali kadhalika, Marekani itaendelea kushirikiana na mamlaka husika Lebanon kuangalia mahitaji gani ya kiafya na kibinadamu yanahitajika na kutoa misaada zaidi.

Shirika la Marekani linaloshughulikia Maendeleo ya Kimataifa limepeleka timu ya kusaidia maafa kusaidia kuratibu na kusambaza misaada, tamko hilo limesema.

Marekani tangu hapo awali iliahidi kutoa zaidi ya dola milioni 17 ya misaada ya dharura kwa nchi hiyo, Waziri wa Mambo ya Nje Michael Pompeo amesema, na “ itaendelea kuwasaidia wananchi wa Lebanon wakati wanaendelea kujinasua kutoka katika maafa haya.”

Na zaidi ya kutoa misaada, Pompeo amesema, Marekani inaungana na mataifa mengine katika wito wa “kuwepo uchunguzi wa kina na uliowazi” juu ya sababu za mlipuko huo.

Wafanyakazi za uokozi wa Umoja wa Mataifa walikuwa wanatafuta walionusurika iwapo wako ndani ya kifusi Ijumaa. Timu za waokoaji kutoka Ufaransa na Russia wakitumia mbwa walikuwa wanatafuta manusura katika eneo hilo siku ya Ijumaa.

Mamlaka nchini Lebanon wanaamini tani 2,750 za kemikali aina ya ammonium nitrite iliyokuwa imehifadhiwa katika maghala kwa kipindi cha miaka sita iliyopita ndio iliyopelekea mlipuko huo wiki hii.

Mlipuko huo uliuwa watu 150, na kujeruhi zaidi ya watu 5,000, na kuwaacha wengine 300,000 bila makazi.

Wakati huohuo, maafisa wa Lebanon wanasema wanatarajia idadi ya vifo kuongezeka wakati wanaendelea kufukua vifusi. Makadirio ya awali ya hasara iliyosababishwa na mlipuko huo ni takriban dola bilioni 15.

Maafisa wa afya Lebanon pia wanahofia kuwa maafa haya yataongeza mlipuko wa COVID-19 kutokana na walioathirika kusongamana hospitalini na wasio na makazi kutafuta hifadhi.

Shirika la haki za binadamu Human Rights Watch lilikuwa la kwanza kutoa wito wa kuwepo uchunguzi huru juu ya mlipuko huo.

Kundi hilo limesema wataalam wa kimataifa ni lazima waruhusiwe kuingia Lebanon ili “kutafuta chanzo na wakuwajibishwa kutokana na mlipuko huo na kupendekeza hatua za kuchukuliwa ili kuhakikisha hili halijirudii tena.”

Russia imepeleka ndege yenye hospitali ya kijeshi wakiwemo madaktari 50. Qatar pia inapeleka hospitali, na Iraq inawapeleka wafanyakazi wa afya na malori yenye mahitaji muhimu.

Tunisia imejitolea kuwaleta wagonjwa nchini mwao kwa ajili ya matibabu na Ujerumani imepeleka timu ya waokoaji na mbwa wenye uwezo wa kutafuta watu waliokwama katika vifusi.

Ahadi za misaada ya kifedha imetolewa na Australia, Uingereza, Hungary na nchi nyingine.

XS
SM
MD
LG