Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatano, Oktoba 04, 2023 Local time: 17:30

Marekani kuendelea kushiriki katika soko la NAFTA


Rais Donald Trump

Ikulu ya White House imesema Jumatano kuwa Trump amekubali kutochukua hatua ya kujitoa katika soko huru la biashara la Amerika ya Kaskazini (NAFTA) baada ya mazungumzo ya simu na viongozi wa Canada na Mexico.

Kabla ya mazungumzo hayo ya simu repoti zilieleza kuwa Rais Donald Trump alikuwa anafikiria kutoa amri ya kiutendaji kuiondosha Marekani katika NAFTA.

Tangu alipotangaza kuwania urais, Trump amerejea mara kwa mara kukosoa makubaliano ya nchi yake ya biashara hasa NAFTA, akisema mikataba iliosainiwa mwaka 1994 ilikuwa ni “janga” na kusababisha ajira nyingi kuhamia Mexico.

“Rais Trump amekubali kutojitoa katika NAFTA wakati huu, na viongozi wote wamekubaliana kuendelea nayo, kwa kufuata taratibu za nchi zao husika, ilikuwezesha mazungumzo mapya ya makubaliano ya NAFTA kufanyika ili kuzinufaisha nchi zote tatu,” White House imesema.

Tamko hilo limeongeza kuwa Trump anaamini ni heshima kubwa kwake kuweza kufanya kazi na Waziri Mkuu wa Canada Justin Trudeau na Rais wa Mexico Enrique Pena Nieto, na ana amini mchakato wa kufanya mazungumzo upya utazifanya nchi hizo tatu kuwa na nguvu zaidi.

Tamko la serikali ya Mexico limethibitisha kuwepo mazungumzo ya simu kati ya Trump na Pena Nieto likisema viongozi hao wamekubaliana juu ya njia nyepesi ya kuendeleza NAFTA na kufanya kazi kwa karibu na Canada ili kufanya mazungumzo hayo yawe yenye mafanikio kwa manufaa ya nchi hizo tatu.

Mapema Jumatano, msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Canada amesema yuko “tayari kufanya mazungumzo wakati wowote.”

Trump ameilenga Canada wiki hii kwa kile alichosema vitendo vya kibiashara visivyo vya haki, na kuamrisha agizo jipya la asilimia 20 la ushuru kwa biashara ya mbao ya Canada inayouzwa nje.

Maafisa wa Mexico wengi wameiita NAFTA ni majuto, wakisema imepunguza kasi ya uchumi kukua pamoja na kuwepo ongezeko la vitega uchumi katika viwanda vidogo na vikubwa.

XS
SM
MD
LG