Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatano, Septemba 18, 2024 Local time: 12:01

Marekani inataka waasi wa M23 kuweka chini silaha, wanaounga mkono waasi wakome mara moja


Waasi wa M23 wakiwa karibu na sehemu iliyowekwa kizuizi cha wamajeshi wa umoja wa mataifa, Kanyaruchinya, kaskazini mwa Goma. May 15,2013
Waasi wa M23 wakiwa karibu na sehemu iliyowekwa kizuizi cha wamajeshi wa umoja wa mataifa, Kanyaruchinya, kaskazini mwa Goma. May 15,2013

Marekani imeshumu mapigano yanayoendelea Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kati ya kundi la waasi la M23 na wanajeshi wa serikali ya DRC na kuwataka waasi kuachilia sehemu wanazozishikilia na kuweka chini silaha.

“Mapigano yamepelekea watu kutaabika, kuuawa na kujeruhiwa huku idadi kubwa ya watu wakikoseshwa makazi,” imesema taarifa ya wizara ya mambo ya nje ya Marekani.

Taarifa hiyo inataka kusitishwa kwa mapigano mara moja na kuheshimiwa kwa haki za binadamu na sheria za kimataifa.

“Tunatoa wito kwa kundi la M23, ambalo liliwekewa vikwazo na Marekani pamoja na Umoja wa Mataifa, kuondoka katika sehemu ambazo wanazishikilia, kuweka chini silaha na kufanya mazungumzo kwa kuunga mkono mchakato wa amani wa Nairobi pamoja na kukubali kuishi maisha ya kawaida kama raia, jinsi ambavyo serikali ya DRC imependekeza.”

Idadi ya wakimbizi imeongezeka

Zaidi ya watu 700,000 wamekoseshwa makazi kutokana na mapigano kati ya kundi la waasi la M23 na wanajeshi wa serikali ya DRC.

Wengi wao wamekimbilia Uganda kama wakimbizi.

Mapigano hayo pia yamepelekea uhusiano kati ya DRC na Rwanda kuendelea kuharibika.

DRC inadai kwamba waasi wa M23 wanasaidiwa na serikali ya Rwanda, huku Rwanda ikidai kwamba jeshi la DRC linasaidiwa na kundi la waasi la FDLR, lenye nia ya kuvuruga usalama wa Rwanda.

Rwanda vile vile imeishutumu DRC kwa kueneza chuki dhidi ya watu wanaozungumza Kinyarwanda, wanaoishi DRC.

Marekani vile vile inataka pande zote ambazo zimetajwa katika mzozo huo, hasa kuliunga mkono kundi la M23 na makundi mengine ya waasi, kuacha kufanya hivyo.

“Tunasikitika kutokana na kuenea kwa ujumbe wa chuki na tunatoa wito wa kumalizwa kwa chuki hizo. Tunahimiza kuanza haraka mazungumzo ya amani ya Nairobi, sawa na ya Luanda katika kutafuta suluhu ya mzozo huo. Wahusika wote katikaJjumuiya ya Afrika Mashariki na Maziwa Makuu lazima waheshimu kanuni zilizokubaliwa na viongozi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na makubaliano ya Luanda.” Imesema taarifa ya wizara ya mambo ya nje ya Marekani.

Licha ya mashambulizi ya jeshi la DRC, waasi wa M23 wamekataa kuachilia sehemu wanazozishikilia, ikiwemo mji wa kibiasha wa Bunagana.

Marekani imeonya kwamba mashambulizi dhidi ya walinda usalama wa Umoja wa Mataifa – MONUSCO – ni hatua itakayopelekea wahusika kuwekewa vikwazo kulingana na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Wanajeshi kadhaa wa Umoja wa Mataifa wamejeruhiwa wakati wakwasaidia wanajeshi wa DRC kulinda amani mashariki mwa nchi hiyo.

XS
SM
MD
LG