Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Mei 27, 2024 Local time: 13:21

Marekani imeamurisha Rwanda kuacha kusaidia kundi la waasi la M23


Rais wa Rwanda Paul Kagame
Rais wa Rwanda Paul Kagame

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Anthony Blinken ameambia rais wa Rwanda Paul Kagame kuacha kutoa msaada kwa kundi la waasi la M23 linalopigana na serikali ya Kinshasa, mashariki mwa Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo.

Taarifa ya wizara ya mambo ya nje ya Marekani inasema kwamba waziri Blinken amefanya mazungumzo ya simu na rais wa Rwanda Paul Kagame na kuzungumzia umuhimu wa kuwepo amani na utulivu mashariki mwa DRC.

Blinken amesema kwamba Marekani inaunga mkono juhudi za amani zinazofanywa na jumuiya ya Afrika mashariki na mpatanishi wa umoja wa Afrika, ambaye ni rais wa Angola Joao Lourenco.

Rwanda imekuwa ikikana kila mara shutuma kwamba inaunga mkono waasi wa M23, lakini taarifa iliyotolewa na msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani Ned Price, inasema kwamba Blinken amesisitiza kwamba “msaada wowote kwa makundi ya waasi yanayopigana Congo lazima ukome mara moja, ikiwemo msaada ambao Rwanda inatoa kwa kundi la waasi la M23.

Rais Paul Kagame amekuwa akisema kwamba Rwanda haihusiki na vita vinavyoendelea nchini Congo, na kwamba kinachofanyika nchini humo ni waasi wanaotaka makubaliano waliofikiwa na serikali ya Kinshasa kutekelezwa.

Marekani na umoja wa mataifa inatambua kundi la M23 kama kundi haramu.

“Waziri Blinken ameelezea kusikitishwa na mapigano yanayoendelea na mauaji yanayotekelezwa na waasi dhidi ya raia,” amesema Ned Price.

Taarifa hiyo haijasema hatua zitakazochukuliwa dhidi ya serikali ya Rwanda endapo itaendelea kusaidia waasi wa M23.

Waasi wa M23 wameshutumiwa kwa kuua raia 50 katika Kijiji cha Kishishe, kivu kaskazini, wiki iliyopita. Waasi hao wamekanusha ripoti kwamba wamehusika na mauaji hayo.

Waasi wa M23 wakiwa katika mji wa Karuba, kilomita 62, magharibi mwa mji wa Goma, Kivu kaskazini, Mashariki mwa DRC
Waasi wa M23 wakiwa katika mji wa Karuba, kilomita 62, magharibi mwa mji wa Goma, Kivu kaskazini, Mashariki mwa DRC

Idadi ya watu waliouawa ‘imeongezeka’

Serikali ya Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo imesema kwamba watu 270 waliuawa katika shambulizi lililotekelezwa na waasi wa kundi la M23 wiki iliyopita.

Hata hivyo, mwenyekiti wa kundi la M23 amefutilia mbali idadi iliyotolewa na serikali na kudai kwamba serikali ya Congo inazusha habari za uongo ili kuwafanya watu kutozingatia maswla ya msingi ikiwemo maovu ambayo yametekelezwa wanajeshi wa serikali na washirika wake.

Msemaji wa serikali Patrick Muyaya amesema kwamba serikali ya Congo imeanzisha uchunguzi kuhusiana na mashambulizi yaliyotokea katika Kijiji cha Kishishe, kilomita 70 kutoka mji wa Goma.

Muyaya amesema kwamba waziri wa sheria wa DRC yupo mjini Hague Uholanzi na amewasilisha kesi ya mauaji hayo kwa mahakama ya uhalifu wa kivita ya ICC ili uchunguzi kuanza kufanyika.

Muyaya ametoa wito kwa waakaazi wa Kishishe, ambapo mauaji yalitokea, akiahidi kwamba waasi wa M23 watalipia gharama ya mauaji hayo.

Awali, serikali ya DRC ilikuwa imesema kwamba watu 50 waliuawa katika shambulizi hilo, na kulaumu waasi wa M23 na wanajeshi wa Rwanda kwa mauaji hayo. Serikali ya Rwanda imekanusha mara kadhaa habari za kusaidia waasi wa M23.

Serikali ya Congo haijafafanua namna imefikia idadi ya watu 270 waliouawa, kutoka kwa 50 iliyokuwa imesema awali lakini msemaji wa serikali amesema kwamba idadi hiyo imetolewa na mashirika ya kiraia katika sehemu hiyo.

Mwenyekiti wa kundi la M23 Bertrand Bisimwa amesema kwamba idadi ya vifo iliyoripotiwa imetoka kwa mkuu wa kundi la wapiganaji la kijamii, na kwamba watu 8 pekee ndio waliouwa kutoka na risasi zilizopigwa bila kukusudia.

XS
SM
MD
LG