Idadi ya vifo kutokana na tetemeko la ardhi la kiwango cha 6.8 kwa kipimo cha rikta lilipiga katika milima ya High Atlas Ijumaa usiku imefikia zaidi ya watu 2,800, huku zaidi ya 2,500 wakijeruhiwa, lakini idadi huenda ikaongezeka.
Waokoaji kutoka Spain, Uingereza, na Qatar walikuwa wanawasaidia waokoaji wa Morocco wakati Italia, Ubelgiji , Ufaransa na Ujerumani wameahidi kupeleka wataalamu lakini wamesema bado hawajapokea kibali kutoka serikali ya Morocco.
Matumaini ya kuwapata manusura wengine chini ya vifusi yalikuwa yanadidimia wakati muda ukienda kwa sababu nyumba nyingi za kitamaduni zilizojengwa kwa matofali ya kuchoma ziliporomoka na kuwa kifusi bila kuacha nafasi yoyote.
Shirika la msalaba mwekundu leo limetoa wito wa msaada wa zaidi ya dola milioni 100 ili kutoa msaada unaohitajika sana nchini Morocco, siku chache baada ya tetemeko kubwa la ardhi kuua karibu watu 2,900.
“Tunatafuta msaada wa dola milioni 112 ili kuweza kusambaza mahitaji muhimu kwa wakati huu,” Caroline Holt, mkurugenzi wa shughuli za kimataifa katika Shirikisho la kimataifa la msalaba mwekundu na Mwezi Mwekundu (IFRC), amewaambia waandishi wa habari mjini Geneva.
Amesema fedha hizo zinahitajika kwa ajili ya “afya, maji, usafi wa mazingira na usafi, vifaa vya misaada vya makazi na mahitaji ya msingi”, akisisitiza kwamba wanahitaji kuhakikisha wanaepuka wimbi la pili la janga.
Timu za uokoaji kutoka Morocco na nje leo zimeendelea kuchimba kwenye vifusi vya nyumba zilizobomolewa za matofali ya udongo, zikitarajia kuwapata watu ambao bado wako hai wakati wakikimbazana na muda.
Tetemeko la siku ya Ijumaa la kiwango cha 6.8 kwa kipimo cha Rikta lilikuwa kubwa sana kuwahi kutokea nchini Morocco.
Lilikuwa tetemeko baya zaidi kupiga taifa hilo la Afrika Kaskazini tangu tetemeko la mwaka 1960 ambalo liliuharibu mji wa Agadir kwenye pwani ya Atlantic na kuua kati ya watu 12,000 na 15,000.
Chanzo cha habari hii ni shirika la habari la Reuters na vyanzo vya habari vingine.
Forum