Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Septemba 10, 2024 Local time: 20:25

Tetemeko la Morocco lauwa zaidi ya watu 2,000, huku Algeria yafungua anga yake


Nyuma iliyoporomoka kufuatia tetemeko kubwa la ardhi nchini Moroko
Nyuma iliyoporomoka kufuatia tetemeko kubwa la ardhi nchini Moroko

Tetemeko kubwa la ardhi lililotokea nchini Moroko limeua zaidi ya watu 2,000 na kujeruhi mamia zaidi, ambalo ni baya zaidi kuwahi kutokea nchini humo kwa zaidi ya miongo sita, limeangusha nyumba katika vijiji vya mbali vya milimani ambako waokoaji walichimba vifusi kuwatafuta manusura.

Wakazi wa kijiji cha Moulay Brahim wahama nyumba zao karibu na kitovu cha tetemeko la ardhi.
Wakazi wa kijiji cha Moulay Brahim wahama nyumba zao karibu na kitovu cha tetemeko la ardhi.

Kitovu cha tetemeko hilo linaripotiwa kuwa katika milima ya Atlas na lilitokea usiku wa kuamkia Jumamosi na kuharibu majengo ya kihistoria ya jiji la Marrakech linalopatikana karibu na milima hiyo. Miji na vijiji katika eneo la tetemeko, kwenye milima Atlas vimeharibiwa vibaya sana.

Wizara ya mambo ya ndani ya Moroko imesema zaidi ya watu 2,000 wamefariki na wengine 672 kujeruhiwa kutokana na tetemeko hilo, lililopimwa na idara ya jiolojia ya Marekani likiwa na nguvu za 6.8 kwenye kipimo cha rikta6.8 na kuwa katika eneo la takriban kilomita 72 kusini magharibi mwa Marrakech.

Watu walala nje kufuatia tetemeko la ardhi kwenye milima ya Atlas nchini Moroko
Watu walala nje kufuatia tetemeko la ardhi kwenye milima ya Atlas nchini Moroko

Katika kijiji cha Amizmiz karibu na eneo hilo waokoaji walikua wakichimba kwenye vifusi kwa mikono yao kutafuta waathiriwa.

"Nilipohisi ardhi ikitetemeka chini ya miguu yangu na nyumba ikielemea upande mmoja nilikimbia kuwatoa watoto wangu. Lakini majirani zangu hawakuweza" alisema Mohamed Azaw.

"Kwa bahati mbaya hakuna mtu aliyepatikana akiwa hai katika familia hiyo. Baba na mwanawe wa kiume walikutwa wamekufa na wanaendelea kuwatafuta mama na binti yao", aliongezea kusema Azaw

Takriban wanaume 20 wakiwemo wafanyakazi wa zima moto nawanajeshi wakiwa na wamevaa sare zao za kazi walisimama juu ya nyumba iliyoharibiwa huko Amizmiz walipokuwa wakijaribu kuondoa vifusi, vipande vya zulia na samani zilizokuwa zinachungulia kwenye mipasuko kati ya sakafu ya saruji.

Mtu ameokolewa kutoka chini ya vifusi katika kijiji cha Moulay Brahim, kufuatia tetemeko kubwa la ardhi.
Mtu ameokolewa kutoka chini ya vifusi katika kijiji cha Moulay Brahim, kufuatia tetemeko kubwa la ardhi.

Tetemeko hilo lililotokea mwendo wa saa 5 usiku liliathiri nyanda za juu za milima ya Atlas. Matetemeko mengine yalitokea katika maeneo mengine ya Huelva na Jaen huko Andalusia kusini mwa Uhispania, televisheni ya Uhispania RTVE iliripoti.

Picha za kamera za mtaani mjini Marrakech zilionyesha wakati ardhi ilipoanza kutikisika, watu walishtuka na kuruka haraka na wengine wakakimbilia kwenye uchochoro na kukimbia huku vumbi na uchafu ukiwazunguka.

Mjini Marrakech, ambako watu 13 walithibitishwa kufariki dunia wakaazi walikaa usiku kucha nje wakiogopa kurudi nyumbani.

Katikati ya jiji lake la zamani wilaya ya Turathi ya Dunia la UNESCO, mnara wa msikiti ulianguka katika uwanja wa Jemaa al-Fna.

Mskiti wa kale ulobomoka katika mji wa Marrakesh kufuatia tetemeko kubwa la ardhi.
Mskiti wa kale ulobomoka katika mji wa Marrakesh kufuatia tetemeko kubwa la ardhi.

Watu waliojeruhiwa walifika hadi Marrakech kutoka maeneo ya karibu wakitafuta matibabu.

Picha za televisheni ya serikali kutoka eneo la Moulay Ibrahim kiasi cha kilomita 40 kusini mwa Marrakech zilionyesha darzeni ya nyumba zimeporomoka chini ya mlima na wakaazi wakichimba makaburi wakati vikundi vya wanawake vikisimama barabarani.

Montasir Itri, mkazi wa kijiji cha Asni karibu na kitovu hicho, alisema nyumba nyingi hapo ziliharibiwa.

“Majirani zetu wapo chini ya kifusi na watu wanafanya kazi kubwa ya kuwaokoa kwa kutumia njia zilizopo kijijini hapo,” alisema.

Upande wa magharibi, karibu na Taroudant, mwalimu Hamid Afkar alisema alikuwa amekimbia kutoka nyumbani kwake na kuhisi mitetemeko midogo baadaye.

“Tetemeko la ardhi lilisababisha mtikiso mkubwa kiasi cha sekunde 20. Milango ilijifungua na kujifunga yenyewe nilipokuwa nikishuka kutoka ghorofa ya pili," alisema.

Huko Marrakech, wakaazi walielezea matukio ya kukatisha tamaa wakati watu wakikimbia kutafuta usalama.

Bado siwezi kulala ndani ya nyumba kwa sababu ya mshtuko na pia kwa sababu mji wa zamani una nyumba za zamani," alisema Jaauhari Mohamed, mkazi wa Old City.

Televisheni ya serikali ya Morocco ilionyesha picha za wanajeshi waliotumwa kusaidia katika juhudi za uokoaji.

Watu katika kijiji cha Moulay Brahim wameanza kuzika jamaa zao kufuatia tetemeko kubwa la ardhi Ijuma usiku.
Watu katika kijiji cha Moulay Brahim wameanza kuzika jamaa zao kufuatia tetemeko kubwa la ardhi Ijuma usiku.

Lilikuwa ni tetemeko baya zaidi kuwahi kutokea nchini Morocco tangu mwaka 1960 wakati tetemeko lilipokadiriwa kuwaua watu wasiopungua 12,000, kwa mujibu wa Utafiti wa Jiolojia wa Marekani. Kwa kina cha kilomita 18.5, wataalam walisema hii ilikuwa tetemeko kubwa lisilo la kawaida kwa eneo hilo.

Uturuki, ambako matetemeko makubwa ya ardhi mwezi Februari yaliua zaidi ya watu 50,000, ilisema iko tayari kutoa msaada.

Algeria, ambayo ilivunja uhusiano na Morocco mwaka jana, ilisema itafungua anga yake kwa ndege za misaada na matibabu.

Matetemeko ya ardhi yenye kina kirefu kwa kawaida yana uharibifu mkubwa," alisema Mohammad Kashani, Profesa wa Uhandisi wa Miundo na Tetemeko la Ardhi katika Chuo Kikuu cha Southampton.

Alilinganisha matukio ya baada ya tetemeko na picha kutoka Uturuki mwezi Februari "Eneo hilo limejaa majengo ya zamani na ya kihistoria, ambayo hasa ni ya uashi. Majengo ya saruji yaliyoimarishwa yalianguka ambayo niliona iyaikuwa ya zamani au ya chini ya kiwango.

Serikali kote ulimwenguni zilionyesha mshikamano na kutoa misaada.

Marrakech inatazamiwa kuwa mwenyeji wa mikutano ya kila mwaka ya Shirika la Kimataifa la Fedha na Benki ya Dunia mapema mwezi Oktoba.

Huko Marrakech, baadhi ya nyumba katika jiji hilo la kale zilibomoka na watu walitumia mikono yao kuondoa uchafu walipokuwa wakisubiri vifaa vizito kufika kuwasaidia alisema mkazi Id Waaziz Hassan.

Watu katika mji mkuu wa Rabat, kiasi cha kilomita 350 kaskazini mwa Ighil, na katika mji wa pwani wa Imsouane, karibu kilomita 180 upande wa magharibi, pia walikimbia makazi yao, wakihofia tetemeko kubwa zaidi.

Mjini Casablanca, takriban kilomita 250 kaskazini mwa Ighil, watu ambao walilala barabarani wakiogopa kurudi makwao.

"Nyumba ilitikisika kwa mshtuko mkubwa, kila mtu alikuwa na hofu," mkazi Mohamed Taqafi alisema.

Forum

XS
SM
MD
LG