Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Septemba 17, 2024 Local time: 17:34

Mahakama ya Tunisia yamruhusu mpinzani wa tatu kugombea urais


Katibu mkuu wa Chama cha CPR Mohamed Abbou (Kulia), alipokuwa akiongea na Imed Daimi, huko Tunis Agost 24, 2012. Picha na AFP
Katibu mkuu wa Chama cha CPR Mohamed Abbou (Kulia), alipokuwa akiongea na Imed Daimi, huko Tunis Agost 24, 2012. Picha na AFP

Mahakama ya Tunisia ilisema Ijumaa kwamba imekubali rufaa ya mgombea urais ambaye uteuzi wake ulikuwa umekataliwa, na hivyo kumruhusu kugombea katika uchaguzi wa Oktoba 6.

Imed Daimi, ambaye aliwahi kuwa mshauri wa rais wa zamani Moncef Marzouki, alikuwa miongoni mwa wagombea 14 waliozuiliwa na mamlaka ya uchaguzi ya Tunisia, ISIE, kugombea.

Hii ni mara ya tatu wiki hii kwa mahakama kubatilisha uamuzi wa mamlaka hiyo wa kumzuia mgombea.

Lakini tume ya ISIE, ambayo inatarajiwa kutoa orodha ya mwisho ya wagombea urais wiki ijayo, bado haijathibitisha kama wataruhusiwa kushiriki kwenye kinyang'anyiro hicho.

Hadi sasa, mamlaka ya uchaguzi imeidhinisha uteuzi wa wagombea watatu, akiwemo Rais wa sasa Kais Saied.

Mahakama imekubali rufaa za waziri wa zamani Mondher Zenaidi, kiongozi wa chama cha upinzani Abdellatif Mekki, na Daimi.

Iwapo wataruhusiwa kugombea, watajiunga na mbunge wa zamani Zouhair Maghzaoui na mfanyabiashara Ayachi Zammel kupambana na Saied.

Daimi, mwenye umri wa miaka 54, ni makamu wa rais wa chama cha upinzani cha Harak, ambacho kiongozi wake aliye uhamishoni, rais wa zamani Marzouki, ni mkosoaji mkubwa wa Saied.

Marzouki alikuwa rais wa kwanza kuchaguliwa nchini Tunisia kufuatia vuguvugu la mwaka 2011 ambalo lilimuondoa madarakani mtawala wa muda mrefu Zine El Abidine Ben Ali na kuchochea maandamano ya Arab Spring katika eneo hilo.

Mwezi Februari, Marzouki alihukumiwa kifungo cha miaka minane gerezani bila yeye kuwepo mahakamani kwa kudaiwa "kusababisha machafuko" nchini Tunisia. Mwaka 2021, alihukumiwa kifungo cha miaka minne kwa kutishia usalama wa taifa.

Saied amemwuta yeye kama "adui wa Tunisia."

Saied alichaguliwa kidemokrasia mwaka 2019 lakini aijilimbikizia madaraka makubwa mwaka 2021. Anawania muhula wa pili, na idadi kadhaa ya wapinzani wake wa kisiasa na wakosoaji wako gerezani au wanakabiliwa na mashtaka.

Wiki iliyopita, Human Rights Watch ilisema kuwa mamlaka ya Tunisia "wamewashtaki, kuwatia hatiani au kuwafunga angalau wagombea wanane watarajiwa" kwa ajili ya uchaguzi wa Oktoba.

Forum

XS
SM
MD
LG