Rais Magufuli wakati akizindua mwaka mpya wa kimahakama nchini unaojulikana kama siku ya sheria alishtukia hekaheka za walinda usalama wakimzuia mama huyo aliyejitambulisha kwa jina la Swabaha Mohamed ambaye ni mkazi wa mkoa wa Tanga.
Mwandishi wa Idhaa ya Kiswahili ameripoti kuwa Magufuli aliwashukia watendaji wa polisi na taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa (Takukuru) kwa madai ya kukwamisha uendeshaji na hukumu za kesi mbalimbali na pia kuvuruga ushahidi.
“Mnakwenda mahakamani mnazungumza upelelezi bado unaendelea, umemshika na jino la tembo, unasema upelelezi unaendelea unataka umshike na nini tena kingine,” rais alihoji.
“Umemshika na madawa ya kulevya, upelelezi unaendelea, mara nyingine yale madawa yanabadilishwa yakishafikishwa kwa mkemia mkuu yalikuwa madawa ya kulevya yakageuzwa kuwa mihogo kutoka sumbawanga…,” alisema.
Mjane huyo amedai kudhulumiwa haki yake ya mirathi ya marehemu mume wake alizua taharuki ghafla katikati ya uzinduzi huo na kutoa malalamiko yake moja kwa moja kwa rais, huku akiwa na vielelezo vya kesi anazodai zimechukua muda mrefu, huku kukiwa na njama pia za kumtoa uhai ili kumdhulumu haki yake.
Uzinduzi wa mwaka mpya wa mahamaka umebeba kauli mbiu ya 'umuhimu wa utoaji haki kwa wakati utakavyowezesha ukuaji wa kiuchumi'.
Taasisi hizo tatu zimetakiwa kushughulikia mara moja kesi ya mjane huyo aliyejitokeza katika mahafali ya siku ya sheria nchini.
“Kama kesi iko mahakama ya mwanzo muivute kutoka huko haraka haraka na ishughulikiwe mara moja,” Rais alitoa amri hiyo.
Pia aliitaka ofisi ya mkuu wa polisi (IGP) ishughulikie kesi hiyo na kumlinda mjane huyo asije akadhulumiwa kwa kitu chochote.