Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Desemba 04, 2023 Local time: 16:21

Magufuli aahidi ajira baada ya 'kutumbua majipu' serikalini


Rais John Magufuli
Rais John Magufuli

Rais John Magufuli ameamrisha kuwa waliokutwa na vyeti vya kughushi nchini Tanzania mishahara yao ikatwe na waondolewe kwenye utumishi wa Umma mara moja.

“Waziri mkuu, hawa watumishi mishahara yao ikatwe na waondolewe kwenye utumishi wa umma mara moja," Rais ameagiza hilo wakati akipokea repoti ya uhakiki wa vyeti vya wafanyakazi wa serikali makao makuu Dodoma.

"Watakaofika na kubisha mpaka mwezi wa tano basi wachukuliwe hatua hata wakafungwe hiyo miaka 7.Hizo nafasi 9,932 zitangazwe ili watu wenye sifa wapate kuzijaza,” Rais amesisitiza.

Rais ametoa angalizo kuwa tarehe ya mwisho kwa wafanyakazi hao walioghushi vyeti kuachia ngazi na iwapo watakuwa hawajaondoka mpaka tarehe 15 Mei, "basi wakuu wa idara waripotini kwenye vyombo vya dola ili wakaseme vyeti vyao walivichapisha wapi."

“Hayo majina yachapishwe kwenye magazeti maana ndio uwazi. Tanzania kuajiriwa sio mpaka uwe na digrii, hata darasa la saba utaajiriwa kulingana na sifa zako. Kila tabaka ya elimu Tanzania unaweza kupata kazi inayokufaa kutokana na ujuzi wako,” Rais alisisitiza.

Rais ameiagiza wizara ya fedha kufuta majina yao kwenye kompyuta, “hata mimi nitakuwa naangalia.”

“Wale wenye vyeti vyenye utata, mpaka tarehe 15 May muwe mmehakikisha wahusika wa vyeti halali. Na mishahara yao kwanza msianze kuwapa mpaka uhakiki ukamilike,” alisema Rais.

Rais amesema kuwa mpaka hapa zoezi lilipokamilika serikali itakuwa imetengeneza nafasi za ajira 12,000, akiongeza kuwa, “si haba.”

Akitoa maagizo zaidi, Rais amesema watumishi 11,569 waliwasilisha vyeti pungufu na hivyo hawa waendelee kulipwa mishahara wakati uchunguzi ukiendelea “tusije tukawanyima watu haki yao.”

Rais aliongeza kuwa watumishi 9,932 kati ya watumishi waliohakikiwa walikutwa na vyeti vya kughushi.

“Tumekuwa tukibezwa sana kuwa kwanini Sensa inachukua muda mfupi lakini uhakiki unachukua muda mrefu lakini ni kwa sababu kazi hii inahitaji umakini,” amesema Waziri wa Utumishi, Angela Kairuki wakati anakabidhi repoti hiyo kwa Rais.

Serikali imekamilisha uhakiki wa wafanyakazi wake mchakato ambao haujawahi kufanyika kwa mkupuo namna hii na umeacha historia ya kipekee.

Kwa mujibu wa kanuni za nchi adhabu ya mtu aliyefanya kosa la kughushi cheti ni kifungo Jela miaka Saba.

Waziri Kairuki amekabidhi ripoti na boksi lenye majina ya watumishi na taarifa zao kamili kama wako wapi na wanapatikana wapi.

Zoezi hilo la kukabidhi repoti lilihudhuriwa na Waziri Mkuu, mawaziri na viongozi mbalimbali wa serikali.

XS
SM
MD
LG