Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumapili, Novemba 27, 2022 Local time: 21:58

Magufuli aomboleza vifo vya wanafunzi


Basi lililokuwa linasafirisha wanafunzi

Rais John Magufuli amesikitishwa na vifo vya ghafla vya wanafunzi wa darasa la saba, walimu na dereva wa gari la shule ya msingi iitwayo Lucky Vincent ya Arusha.

Taarifa ya Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu ilieleza kwa masikitiko Rais Magufuli amemtumia salamu za rambirambi Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo na kueleza kuwa ajali hiyo imezima ndoto za watoto waliokuwa wakijiandaa kulitumikia Taifa na imesababisha uchungu, huzuni na simanzi kubwa kwa familia za marehemu na Taifa kwa ujumla.

“Ndugu Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mrisho Gambo naomba unifikishie pole nyingi kwa wazazi, ndugu, jamaa na marafiki wote wa wanafunzi, walimu na dereva waliopoteza maisha, hiki ni kipindi kigumu kwetu sote, na uwaambie naungana nao katika majonzi na maombi,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.

Taarifa hiyo imesema kuwa vifo hivyo vilitokea jana saa tatu asubuhi baada ya gari walilokuwa wakisafiria kupata ajali katika eneo Rhotia Marera, Wilaya ya Karatu Mkoani Arusha.

Rais aliongeza kusema kuwa, “muhimu kwa sasa tuwaombee marehemu wote wapumzishwe mahali pema, majeruhi wapone haraka na wote walioguswa na msiba huu wawe na moyo wa subira, ustahimilivu na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu.”

Spika wa Bunge

Wakati huo huo, Spika wa Bunge Job Ndugai ametuma salamu za rambirambi kwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo kutokana na vifo vya wanafunzi, walimu na dereva wa Shule ya Msingi Lucky Vicent ya mkoani Arusha.

Ajali hiyo ilitokea baada ya gari walilokuwa wakisafiria kupata ajali jana asubuhi katika eneo la Rhotia Marera, wilayani Karatu, mkoani Arusha.

“ Mkuu wa Mkoa nakupa pole sana, nimepokea kwa mshtuko taarifa hii ya ajali iliyogharimu maisha ya watoto wetu, hakika hili ni pigo kwa taifa zima, namuomba Mungu azilaze roho za marehemu mahali pema peponi,” alisema Ndugai.

Aliongeza kuwa, “natoa pole kwa familia, ndugu, jamaa na marafiki waliopoteza wapendwa wao, Mwenyezi Mungu awape nguvu na faraja katika kipindi hiki kigumu, vilevile nawaombea majeruhi wote wa ajali hiyo wapate uponyaji wa haraka.”

Katika hatua nyingine, Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe, amesema chama chake kimepokea kwa majonzi na simanzi kubwa taarifa ya vifo vya wanafunzi pamoja na waalimu wao.

Taarifa kwa vyombo vya habari Zitto zimsema taifa limepoteza nguvu kazi ambayo si rahisi pengo lake kuzibwa na kuwapa pole waalimu wa shule ya awali na Msingi ya Lucky Vicent, wazazi wa watoto, ndugu, jamaa na marafiki ambao wamepoteza vipenzi vyao.

Kiongozi huyo wa ACT aliomba kwa Mwenyezi Mungu majeruhi wapone haraka na waweze kuendelea na masomo yao mpaka wafikie malengo waliyotarajiwa. “ACT- Wazalendo tumesikitishwa na vifo hivi vya watoto wetu pamoja na walimu wao, tunawapa pole ndugu jamaa na marafiki Mwenyezi Mungu awape nguvu ya kuhimili kipindi hiki kigumu kwao… Mwenyezi Mungu aziweke roho za marehemu mahali pema peponi, Amini,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.

Vyanzo vya habari nchini Tanzania vimeripoti kuwa wazazi wameonekana wakitambua miili katika hospitali ya Mount Meru.

XS
SM
MD
LG