Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Machi 19, 2024 Local time: 09:22

Magufuli aamrisha kifo cha mwanafunzi kichunguzwe


Rais John Magufuli
Rais John Magufuli

Vyombo vya dola nchini Tanzania vimeagizwa na Rais kuchunguza na kuwachukulia hatua waliosababisha kifo cha mwanafunzi wa chuo cha usafirishaji Tanzania (NIT) Akwilina Akwiline

"Nimesikitishwa sana na kifo cha mwanafunzi Akwilina Akwilini wa Chuo cha Usafirishaji (NIT). Natoa pole kwa familia,ndugu,wanafunzi wa NIT na wote walioguswa na msiba huu. Nimeviagiza vyombo vya dola kufanya uchunguzi na kuwachukulia hatua za kisheria waliosababisha tukio hili," Rais John Magufuli aliandika kwenye akaunti yake ya Twitter.

Mwanafunzi aliyeuwawa jina lake na picha tayari viko katika mitandao ya kijamii baada ya kupigwa risasi akiwa ndani ya basi dogo maarufu kama daladala jijini Dar es salaam.

Vyama vya kisiasa na jumuiya ya wanafunzi zimetoa tamko kushinikiza wale wote waliosababisha kifo hicho kuchukuliwa hatua na kutaja majina ya baadhi ya viongozi kuwajibika.

Tukio hilo lilitokea siku ya Ijumaa majira ya jioni, ikiwa siku moja kabla ya uchaguzi mdogo wa ubunge katika eneo la kinondoni kufanyika.

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba ametakiwa kujiuzulu ili kuonyesha uwajibikaji kwa maelezo kuwa ameshindwa kusimamia amani.

Wakati huo huo Mtandao wa wanafunzi Tanzania (TSNP) na Chama cha ACT-Wazalendo wametoa kauli hiyo Jumapili ikiwa ni siku moja baada ya kupigwa risasi kwa mwanafunzi wa Chuo cha Usafirishaji cha Taifa (NIT), Akwilina Akwiline.

Kwa upande wao Chama cha ACT Wazalendo kimemtaka Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba awajibike kwa kujiuzulu wadhifa wake kwa sababu ameshindwa kukomesha mfululizo wa mauaji ya watu wasio na hatia.

Pia, wamewataka Mkuu wa Jeshi la Polisi, IGP Simon Sirro na Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa nao wajiuzulu kwa kushindwa kutekeleza majukumu yao ikiwamo kulinda usalama wa raia na mali zao.

XS
SM
MD
LG