Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Machi 28, 2024 Local time: 14:42

Viongozi 7 wa Madaktari Wafungwa Mwezi Mmoja


Ouma Oluga, Katibu Mkuu wa Chama cha Taifa cha Madaktari akihutubia madaktari wakati wakiendelea na mgomo
Ouma Oluga, Katibu Mkuu wa Chama cha Taifa cha Madaktari akihutubia madaktari wakati wakiendelea na mgomo

Viongozi saba wa madaktari wamehukumiwa kifungo cha mwezi mmoja kwa kupuuza amri ya mahakama. Hakimu wa mahakama ya viwanda na wafanyakazi wa umma Hellen Wasilwa ametoa hukumu hiyo Jumatatu mjini Nairobi, Kenya.

Mwandishi wa idhaa ya Kiswahili VOA ameripoti kuwa hakuna ishara yoyote ya kupatikana kwa mwafaka katika sakata hilo liliopo kati ya madaktari na Serikali.

Mgomo wa madaktari tayari umeingia siku ya 71 Jumatatu wakati mahakama ya viwanda na wafanyakazi Nairobi ilipotoa hukumu hiyo.

Miongoni mwa waliofungwa ni Mwenyekiti wa Chama cha Taifa cha Madaktari, Samuel Oroko, Katibu Mkuu Ouma Oluga, Mweka Hazina Daisy Korir na maafisa wengine wanne ambao wataendelea kutumikia kifungo cha mwezi mmoja gerezani.

Madaktari sasa wanaapa kukatiza mazungumzo yoyote hadi wenzao saba waliofungwa waachiliwe. Pia wanasema wamechukizwa jinsi ambavyo serikali imekuwa ikishughulikia matakwa ya madaktari.

Wiki moja iliyopita mahakama hiyo ilikuwa imeagiza kuwa Katibu Mkuu wa chama cha wafanyakazi Francis Atwoli kuingilia kati mgogoro huu na kuzileta pamoja pande kinzani kutafuta ufumbuzi.

Pia mahakama ilimtaka Atwoli kuikabidhi ripoti ya mazungumzo. Lakini Bwana Atwoli anasema kuwa mgogoro wa madaraka kati ya Waziri wa Afya Cleopas Mailu na Katibu wa wizara hiyo Nicholas Muraguri umekwamisha juhudi za kupata mwafaka.

Aidha, Bwana Atwoli anasisitiza kuwa viongozi wa madaktari na maafisa wa serikali katika mazungumzo wanaendelea kushikilia misimamo mikali ambayo imekuwa ni pingamizi katika kufikia makubaliano kati ya pande hizo mbili.

Lakini leo jinsi ilivyotarajiwa, Hakimu Hellen Wasilwa hakuchelea kutoa uamuzi aliokuwa ameahidi kuutoa wiki iliyopita, akiwalaumu viongozi wa madaktari kwa kupuuza waziwazi amri ya mahakama kusitisha mgomo ambao umeathiri pakubwa sekta ya afya nchini.

Imetayarishwa na Mwandishi wetu Kennedy Wandera, Kenya

XS
SM
MD
LG