Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatano, Aprili 24, 2024 Local time: 09:45

Uganda Yapeleka Kikosi Maalum Kudhibiti Kisiwa cha Migingo


Rais Yoweri Museveni
Rais Yoweri Museveni

Kikosi maalum cha Jeshi la Uganda (SFC) chenye jukumu la kumlinda Rais Yoweri Museveni wa Uganda, kimepelekwa kwenye kisiwa chenye utata cha Migingo ili kudhibiti uvuvi haramu, mpakani mwa Uganda na Kenya.

Mwandishi wa Idhaa ya Kiswahili VOA ameripoti kuwa katika kikao na waandishi wa habari jijini Kampala Jumatatu, msemaji wa Polisi, Andrew Felix Kaweesi, amesema polisi wa majini wameondolewa kisiwani hapo na sasa ulinzi kwenye kisiwa hicho ni kazi ya kikosi maalum cha SFC.

Ameelezea kuwa rais Museveni amekuwa akidai kwamba polisi wamekuwa wakihongwa na wavuvi hasa kutoka Kenya, ambao walikuwa wanavua samaki wachanga, pamoja na kufanya uchafuzi katika ziwa Victoria kinyume cha sheria.

Kikosi hicho cha jeshi, ndicho kinachosimamia ulinzi wa rais nchini Uganda na pia kuhakikisha kuwepo ulinzi imara wa wageni mashuhuri wanapozuru Uganda, na mtindo wake wa kazi unajulikana kuwa wa kukosa mahojiano wala mjadala.

Hatua ya wanajeshi kulinda kisiwa cha Migingo katika ziwa Victoria, ni uamuzi wa Rais Museveni, licha ya kuwepo utata kuhusu umiliki wake, kati ya Uganda na Kenya, huku Kenya ikitaka Uganda kuondoa majeshi yake.

Kaweesi amethibitisha kuwa tayari polisi wa Uganda wamekwisha ondolewa kwenye kisiwa hicho na wanajeshi ndio wanaofanya doria.

Tayari polisi wa Uganda wanaripotiwa kuondolewa kwenye kisiwa hicho na wanajeshi kushika doria, Rais Museveni akidai kwamba polisi wake wamekuwa wakihongwa na wavuvi hasa kutoka Kenya, anaodai wanavua samaki wachanga, pamoja na kufanya uchafuzi katika ziwa Victoria.

Wanajeshi hao pia watashika doria katika mito na maziwa mengine yaliyoko nchini Uganda sawa sawa na kinachofanyika mipakani, amesema msemaji huyo.

Akielezea historia fupi ya kisiwa hicho Kaweesi amewaambia waandishi kuwa umiliki wa kisiwa cha Migingo ziwani Victoria, umekumbwa na matatizo ya muda mrefu kati ya Uganda na Kenya, huku zoezi zima la kutambua mipaka hiyo ikigonga ukuta.

Kisiwa cha Migingo kinaripotiwa kuwa na utajiri mkubwa wa samaki. Mwaka 2011, Rais Museveni alisema kwamba kisiwa cha migingo kipo nchini Kenya lakini maji yanayokizunguka ni mali ya Uganda.

Imetayarishwa na Mwandishi wetu Kennes Bwire, Uganda.

XS
SM
MD
LG