Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Septemba 10, 2024 Local time: 11:25

Madaktari Kenya wamaliza mgomo wa siku 56


Katibu mkuu wa Muungano wa Madaktari, Wafamasia na Madaktari wa Meno KMPDU Dkt Ouma Oluga (kushoto) akiwa na Dkt Samuel Oroko (katikati) na Dkt Allan Ochanji (kulia) wakisindizwa na pingu mikononi Februari 13, 2017. Picha na AFP
Katibu mkuu wa Muungano wa Madaktari, Wafamasia na Madaktari wa Meno KMPDU Dkt Ouma Oluga (kushoto) akiwa na Dkt Samuel Oroko (katikati) na Dkt Allan Ochanji (kulia) wakisindizwa na pingu mikononi Februari 13, 2017. Picha na AFP

Mgomo wa siku 56 wa madaktari katika hospitali za umma nchini Kenya, hatimaye wafikia muafaka, baada ya kufanya makubaliano na serikali siku ya Jumatano, na kutia saini mkataba wa kurejea kazini mara moja licha ya kutofikia muafaka kuhusiana na mishahara ya madaktari wanafunzi.

Muungano wa Madaktari, Wafamasia na Madaktari wa Meno KMPDU ambao unawakilisha zaidi ya madaktari 7,000, umetangaza kufikia muafaka katika utekelezaji kamili wa mkataba wa pamoja wa maafikiano wa mwaka 2017. Na hivyo kuumaliza mgomo huo baada makubaliano yaliyotiwa saini kwenye ukumbi wa Jumba la Kimataifa la Mikutano la Kenyatta, KICC, jijini Nairobi.

Katibu mkuu wa chama cha madaktari KMPDU, Dkt Davji Atellah, amesema kuwa kutiwa saini mkataba wa kurejea kazini mara moja ni njia pekee ya serikali katika kutekeleza kikamilifu mkataba huo wa pamoja wa maafikiano wa mwaka 2017 unaojumuisha masuala mbalimbali yakiwemo uajiri na ulipaji wa mshahara wa kila mwezi kwa madaktari wanafunzi.

Mkataba huo pia unajumuisha upanuzi wa mikataba ya wafanyakazi chini ya mfumo wa afya kwa wote, malipo ya ada kwa madaktari kwenye mafunzo ya uzamili, malipo ya malimbikizo ya mishahara ya kimsingi kulingana na CBA ya 2017 na Utoaji wa Bima ya matibabu ya kina kwa madaktari.

Ingawa madaktari hao wamekubari kutia saini mkataba wa kurejea kazini mara moja, lakini hakuna muafaka uliofikia kuhusiana na mshahara wa kila mwezi wa shilingi elfu 206,000, wa madaktari wanafunzi.

Madaktari hao wamesisitiza kuwa maafikiano yaliyopo si ya kuiruhusu serikali kuwalipa wanafaunzi hao kitita cha shilingi elfu 70,000 ambacho serikali imeahidi kulipa kila mwezi na kisha kuwapa ajira, bali ni kusubiri kesi iliyowasilishwa mahakamani kukamilika.

Madaktari nchini Kenya wakiwa katika mgomo nje ya jengo la makao makuu ya wizara ya afya mjini Nairobi Aprili 9, 2024.
Madaktari nchini Kenya wakiwa katika mgomo nje ya jengo la makao makuu ya wizara ya afya mjini Nairobi Aprili 9, 2024.

Waziri wa Afya Susan Wafula Nakhumicha, amesema kuwa serikali imeahidi kulipa malimbikizo ya msingi ya mishahara, ufadhili wa masomo ya shahada ya kwanza, na bima ya matibabu, lakini haijaridhia kuwalipa madaktari wanafunzi mshahara hadi mahakama itakapotoa uamuzi wa kesi hiyo.

Aidha, ameeleza kuwa imelegeza msimamo wake na kukubali kuwasilisha shilingi bilioni 6.1 kutatua masuala 18 kati ya 19 yaliyoibuliwa na madaktari kwenye mgomo huo.

Kwa ujumla ya madaktari 10,102 waliosajiliwa chini ya KMPDU, 1,200 walioajiriwa na serikali, na 4,480 wanaohudumu katika hospitali za serikali za majimbo, serikali imeahidi kuwapa mpango ulioboreshwa wa bima ya matibabu ifikapo tarehe 1 Julai 2024.

Nakhumicha, akiwa na wakuu wengine wa serikali pamoja na baraza la magavana, amesema kuwa kufika kwa madaktari mezani kumaliza makubaliano hayo, kunapisha majadiliano ya kina kutimiza malengo ya mfumo wa afya kwa wote, hivyo serikali itatilia maanani utekelezaji wa maafikiano yaliowekwa.

Kutia saini mkataba wa kurejea kazini mara moja kunatokana na agizo la jaji Byram Ongaya wa mahakama kuu, kuziagiza pande hizo mbili kuhitimisha majadiliano, kutia saini mkataba wa kurejea kazini kabla ya Jumatano wiki hii.

Madaktari nchini Kenya wakiimba wakati wa maandamano katika mji kuu wa Nairobi April 9, 2024. Picha na SIMON MAINA / AFP.
Madaktari nchini Kenya wakiimba wakati wa maandamano katika mji kuu wa Nairobi April 9, 2024. Picha na SIMON MAINA / AFP.

Majadiliano hayo mara kwa mara yameibuka wakati pande husika zimechukua misimamo mikali, na kuilazimisha mahakama kuingilia kati kuondoa mahangaiko yanayoendelea kushuhudiwa katika hospitali za umma.

Siku nne zilizopita, maafisa wa serikali walijikuta peke yao baada ya viongozi hao wa madaktari kususia kikao hicho kilichokuwa kimeratibiwa kusitisha mgomo huo na kukariri kuwa ni lazima serikali iweke makubaliano ya kuanza kutekeleza mara moja uwasilishaji wa mshahara wa kimsingi wa kila mwezi wa shilingi 206,000 kwa madaktari wanafunzi.

Kwa hilo, madaktari wamelegeza msimamo na kurudi kazini.

Alex Manyasi, mfuatiliaji wa sera na utendakazi wa serikali, anaeleza kuwa serikali inastahili kutekeleza maafikiano yanayowekwa ili kuiepusha nchi mahangaiko kama haya yalioshuhudiwa.

Imetayarishwa na Kennedy Wandera, Sauti ya Amerika, Nairobi

Forum

XS
SM
MD
LG