Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Mei 24, 2024 Local time: 10:39

Koffi Olomide afukuzwa Kenya na Visa yake kufutiliwa mbali


Koffi Olomide congolese musician
Koffi Olomide congolese musician

Mwanamuziki maarufu wa asili ya Congo, Koffi Olomide, siku ya Jumamosi alifukuzwa kutoka Kenya na serikali ya nchi hiyo baada video iliyomuonyesha akimpiga teke mmoja wa wacheza densi wake kulaaniwa vikali, hususan na Wakenya mitandaoni.

Na BMJ Muriithi

Mwanamuziki maarufu wa mitindo ya Lingala, Koffi Olomide, ambaye majina yake kamili ni Antoine Christophe Agbepa Mumba, siku ya Jumamosi alifukuzwa kutoka Kenya na serikali ya nchi hiyo baada video iliyomuonyesha akimpiga teke mmoja wa wacheza densi wake kulaaniwa vikali, hususa na Wakenya mitandaoni.

Serikali ya Kenya ilisema Ijumaa kuwa Visa ya mwanamuziki huyo ya kuingia Kenya ilikuwa imefutiliwa mbali na onyesho lake lililokuwa likisubiriwa na mashabiki wengi pia likafutwa.

Punde tu baada ya kufanya mahojiano na kituo cha televisheni cha Citizen mjini Nairobi Ijumaa jioni, mwanamuziki huyo mwenye umri wa miaka 60 alikamatwa nje ya studio za Royal Media Services kwenye barabara ya Dennis Pritt na kupelekwa moja kwa moja hadi uwanja wa ndege wa Jomo Kenyatta International Airport (JKIA) ambako aliwekwa rumande usiku kucha hadi Jumamosi asubuhi.

Hatimaye Olomide na timu yake walilazimishwa kuabiri ndege ya Kenya Airways na kuondoka nchini humo kuelekea mjini Kinshasa, Jamhuri ya Kidemoktrasia ya Kongo.

Kwa mujibu wa gazeti la Daily Nation, mwanamuziki huyo alibebwa na ndege nambari KQ554 kuelekea Kinshasa, na ambayo iliondoka JKIA mwendo wa saa 11:30 asubuhi.

Taarifa iliyotolewa na serikali ya Kenya ilisema kuwa mwanamuziki huyo angeondolewa nchini Kenya na hati yake ya visa kuingia Kenya, kufutiliwa mbali milele.

Olomide alitiwa nguvuni kufuatia malalamiko makubwa nchini humo baada ya mwanamuziki huyo kushuhudiwa akimpiga teke densa wake katika uwanja wa ndege wa Jomo Kenyatta mapema Ijumaa.

Baada ya Wakenya wengi kuelezea kustaajabishwa kwao na kitendo hicho, Inspekta Mkuu wa Polisi wa kenya Joseph Boinnet aliamuru mwanamuziki huyo akamatwe na awekwe rumande.

Aidha tume ya taifa ya usawa wa kijinsia nchini Kenya ilitoa rai kwa polisi nchini humo kumkamata mwanamuziki huyo, nyota wa muziki wa Lingala, kutokana na kitendo hicho.

Mwanamuziki wa Congo Koffi Olomide

Mwenyekiti wa tume wa usawa wa jinsia Winfred Lichuma alisema kitendo hicho kimesababisha hasira kubwa miongoni mwa wananchi ambao wamechukizwa na kitendo cha mwanamuziki huyo.

Alisema mwanamuziki huyo hana budi kukamatwa na kushughulikiwa kulingana na sheria za Kenya endapo atakutwa na hatia katika kosa hilo. Alisema pia Olomide anatakiwa kuomba samahani hadharani.

Adhabu ya mtu anayekutwa na hatia ya kumpiga mtu mwingine ni kosa dogo la jinai ambayo adhabu yake inaweza kuwa hata mwaka mmoja.

Olomide alitazamiwa kufanya onyesho la muziki katika uwanja wa Bomas Jumamosi usiku, lakini onyesho hilo likafutiliwa mbali.

Katika majojiano yake na Citizen TV Olomide alikanusha kuwa alimpiga teke densa wake huyo - ambaye amemtaja kama Pamela - na kwamba badala yake alikuwa anajaribu kumlinda densa huyo kutoka kwa mwizi wa mfukoni aliyekuwa akimkaribia.

Akizungumza katika mahojiano hayo densa huyo - Pamela - alithibitisha maelezo ya Olomide na kukana kwamba alipigwa na mwanamuziki huyo.

Kufukuzwa nchini kwa mwanamuziki huyo kulikaribishwa kwa furaha na baadhi ya Wakenya, huku baadhi yao wakisema kuwa litakuwa funzo kwa watui ambao hawaheshimu haki za wanawake.

XS
SM
MD
LG