Polisi wa Kenya wamemtia nguvuni mwanamuziki mashuhuri wa Congo Koffi Olomide Ijumaa jioni kufuatia malalamiko makubwa nchini humo baada ya mwanamuziki huyo kushuhudiwa akimpiga teke densa wake katika uwanja wa ndege wa Jomo Kenyatta mapema Ijumaa.
Olomide alikamatwa nje ya kituo kituo cha televisheni cha Citizen TV ambako alikuwa amemaliza mahojiano. Inspekta Mkuu wa Polisi wa kenya Joseph Boinnet alilaani kitendo cha mwanamuziki huyo na kutaka awekwe ndani.
Ripoti pia zimesema kuwa tume ya taifa ya usawa wa kijinsia nchini Kenya ilitoa rai kwa polisi nchini humo kumkamata mwanamuziki huyo, nyota wa muziki wa Lingala, kutokana na kitendo hicho.
Mwanamuziki huyo alionekana katika kanda ya video akimpiga teke mmoja kati ya madensa wake muda mfupi baada ya kutua katika uwanja wa ndege ya Jomo Kenyatta Ijumaa asubuhi.
Mwenyekiti wa tume wa usawa wa jinsia Winfred Lichuma alisema kitendo hicho kimesababisha hasira kubwa miongoni mwa wananchi ambao wamechukizwa na kitendo cha mwanamuziki huyo.
Alisema mwanamuziki huyo hana budi kukamatwa na kushughulikiwa kulingana na sheria za Kenya endapo atakutwa na hatia katika kosa hilo. Alisema pia Olomide anatakiwa kuomba samahani hadharani.
Adhabu ya mtu anayekutwa na hatia ya kumpiga mtu mwingine ni kosa dogo la jinai ambayo adhabu yake inaweza kuwa hata mwaka mmoja.
Olomide alitazamiwa kufanya onyesho la muziki katika uwanja wa Bomas Jumamosi usiku.
Katika majojiano yake na Citizen TV Olomide alikanusha kuwa alimpiga teke densa wake huyo - ambaye amemtaja kama Pamela - na kwamba badala yake alikuwa anajaribu kumlinda densa huyo kutoka kwa mwizi wa mfukoni aliyekuwa akimkaribia.
Akizungumza katika mahojiano hayo densa huyo - Pamela - alithibitisha maelezo ya Olomide na kukana kwamba alipigwa na mwanamuziki huyo.
Boinnet amekaririwa akisema uchunguzi unaendelea. Mpaka sasa haijafahamika kama mwanamuziki huyo ataendelewa kushikiliwa nchini Kenya ama atarudishwa nyumbani DRC haraka iwezekanavyo.