Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Februari 09, 2023 Local time: 05:07

Kituo cha Sheria Tanzania kuomba tafsiri ya 'uchochezi' mahakamani


Dkt Helen Kijo-Bisimba

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), kimetangaza azma yake ya kwenda mahakamani kutafuta tafsiri ya ‘uchochezi’ kisheria.

Pia kituo hicho kimesema kinatarajia kutoa taarifa kwa vyombo vya habari vya kimataifa vinavyohusika na uangalizi wa haki za binadamu, kuomba waingilie kati suala la uhuru wa kujieleza nchini.

Tamko hili limetolewa baada ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kuvipiga faini vituo vitano vya runinga kwa kile kinachodaiwa kukiukwa kwa kanuni za maudhui ya utangazaji,

Akitoa tamko hilo kwa waandishi wa habari Dar es Salaam wiki hii, Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Dkt Helen Kijo-Bisimba, amesema wako tayari kuungana na wadau wengine kwenda mahakamani kuomba tafsiri ya neno uchochezi na baadhi ya vifungu vya kanuni ya maudhui kifungu namba nane.

Kadhalika Dkt Bisimba alisema kuwa wameanzisha harambee ya kuchangia gharama ya kuvisaidia vyombo vya habari vilivyopatiwa adhabu ambayo wao wanaiona kuwa ni uonevu si tu kwa vyombo husika, bali pia kwa uhuru wa kujieleza kwa ujumla.

“Tunaitaka Serikali kuheshimu Katiba iliyopo kwa kutokuingilia uhuru wa kujieleza. Ikubali mazuri na mabaya na kuyatumia maoni ya wananchi wake katika kuipatia Tanzania maendeleo endelevu.

Tunawaomba Watanzania kuungana kuitaka Serikali kutokuchezea uhuru wetu wa kujieleza ambao upo kwa mujibu wa Katiba. Tusiposema sasa tutanyamazishwa kabisa,” alisema Bisimba.

Aidha mkurugenzi huyo alisema kuwa wameiandikia barua TCRA kuitaka kufanya semina kwa LHRC na taasisi nyingine kuhusu namna bora ya kuandaa maudhui.

Vyanzo vya habari nchini Tanzania viliripoti kuwa Novemba 30 mwaka jana, LHRC ilitoa taarifa kwa vyombo vya habari juu ya tathmini ya uchaguzi mdogo wa madiwani uliofanyika katika kata 42 katika maeneo mbalimbali nchini.

Kamati ya Maudhi ya TCRA juzi ilivipiga faini vituo vya ITV, EATV, Channel Ten, Azam Two na Star TV vikidaiwa kuwa Desemba 6 mwaka jana viliripoti habari zilizokosa sifa za kimaadili ambazo zingeweza kuhatarisha usalama wa Taifa.

Facebook Forum

XS
SM
MD
LG