Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Juni 18, 2024 Local time: 15:50

Uchumi kigezo muhimu katika uchaguzi wa Kenya


Shughuli za kilimo cha kahawa huko Gericho nchini Kenya
Shughuli za kilimo cha kahawa huko Gericho nchini Kenya

Zikiwa zimebaki chini ya wiki mbili kabla ya uchaguzi mkuu nchini Kenya, uchumi wa nchi hiyo ya Afrika Mashariki umepewa kipaumbele na wagombea wa urais katika harakati zao za kunadi sera kwa wananchi ambao ni wapiga kura.

Uchumi wa Kenya umeendelea kuimaraika licha ya kuwepo kwa athari ya kujikokota kwa ukuaji wa uchumi duniani. Hata hivyo, wachambuzi wa uchumi na siasa Kenya wanaeleza kuwa kufungwa kwa makampuni ya kibiashara na benki nchini humo ni kiashiria kuwa upatikanaji wa kazi umekuwa adimu.

please wait

No media source currently available

0:00 0:06:01 0:00

Kwa mujibu wa takwimu za Kenya, uchumi wake ulikua kwa asilimia 5.9, asilimia 6.2 na asilimia 5.7 katika robo ya kwanza, ya pili na tatu ya mwaka 2016 mtawalia na kufanikisha ukuaji wa wastani wa asilimia 5.9. Mwaka huu serikali ya Kenya inakadiria uchumi wake kukua kwa zaidi ya asilimia 6.4 lakini ukuaji huu huenda ukakwama iwapo hali ya ukame itaendelea kushuhudiwa kuathiri uzalishaji wa chakula na umeme.

Kenya ni kitovu cha biashara na fedha katika ukanda wa Afrika Mashariki. Lakini kutokana na mpandashuko ulioshuhudiwa baada ya uchaguzi mkuu wa 2008 uliokumbwa na ghasia za baada ya uchaguzi pamoja na kuwepo athari za kutikisika kwa uchumi wa dunia, Kenya ilionekana kujikokota sana.

Na huu ukiwa ni mwaka wa uchaguzi mkuu, wachambuzi wa uchumi na siasa nchini wanaeleza kuwa uchumi ni kigezo muhimu katika uchaguzi huu kwa misingi kuwa kila mkenya atakuwa anawapigia darubini wagombeaji wa urais kufanikisha mustakabali wa nchi kuafikia ruwaza ya mwaka 2030.

Kenya imekuwa ikikumbana na hali ngumu hususan baada ya mashirika na makampuni makubwa nchini kutangaza kuhama Kenya na vile vile kupunguza idadi ya wafanyakazi. Hata hivyo, mtaalamu wa masuala ya siasa Dunstan Omari anaeleza kuwa Rais atakayekuwa madarakani kwa miaka mitano ijayo atakuwa na kibarua kigumu kuboresha uchumi wa Kenya.

Mchumi Aly Khan Sachu anaeleza kuwa athari za gharama ya maisha imewafanya wagombea hawa nane wa urais kuupa uchumi kipaumbele katika uchaguzi mkuu huku akisisitiza kuwa itakuwa vigumu mno kwao kutovisikiliza vilio vya wananchi.

“Uchumi ni muhimu sana leo katika maamuzi ya kura.Uchumi unafuatiliwa na wakenya wengi wanaondelea kuathirika na bei ghali za bidhaa muhimu nchini na katika mazingira hayo, watu huathirika sana iwapo hilo halipewi kipaumbele.”

Serikali ya Jubilee inaeleza kurahisisha upatikanaji wa kazi milioni 1.3 kila mwaka na kuweka angalau kiwanda kimoja katika kila jimbo. Pia, Rais Kenyatta anaeleza kuwa iwapo atapewa awamu ya pili madarakani atafanikisha ujenzi wa makao bora 500,000 kote nchini kwa miaka mitano ijayo kwa ushirikiano na mashirika ya kifedha na kupunguza gharama ya ujenzi kwaasilimia 50% huku akieleza kuwa hali hii itamfanya kila mkenya kujivunia nchi yake.

Kinara wa Upinzani Raila Odinga kupitia manifesto yake anaeleza kuwa kilimo ndio nguzo kuu ya taifa na hivyo basi ili pawe na chakula cha kutosha Kenya haifai tu kutegemea kilimo cha mvua. Aidha, Bw Odinga, anasisitiza kauli kuwa hali ngumu ya maisha imewabana wakenya kutokana na mkakati wa serikali kuendelea kuongeza madeni ya taifa hali ambayo anahisi inaendelea kudunisha mustakabali wa nchi.

Na kupitia ugunduzi wa vipimo vikubwa vya visiwa vya mafuta na gesi katika maeneo ya Turkana Kaskazini Mashariki ya Kenya, taifa linatarajiwa kuimarisha uchumi wake siku za usoni baada ya uchaguzi mkuu.

XS
SM
MD
LG