Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Mei 27, 2024 Local time: 12:20

Kenya yatangaza nyongeza ya mshahara ya 12% kwa wafanayakazi


Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta
Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta

Serikali ya Kenya imetangaza nyongeza ya asilimia 12 kwa wanaolipwa mshahara wa chini kabisa katika sekta zote.

Tangazo hilo lilitolewa Jumapili na Rais Uhuru Kenyatta katika uwanja wa Nyayo, mjini Nairobi, wakati wa sherehe za Leba Dei za mwaka huu.

Kenyatta alisema serikali yake inaelewa changamoto zinazokabili wafanyakazi.

Nyongeza hiyo hata hivyo ni ndogo kuliko matarajio ya muungano wa vyma vya wafanyakazi wa Kenya, COTU, ambacho kilikuwa kimependekeza nyongeza ya 23% .

Tangu janga la Corona kuanza mwezi Machi 2020, gharama ya maisha imeendelea kupanda, na bidhaa muhimu za kimsingi kama vile vyakula kuwa vigumu kupata.

Hali kadhalika bei ya mafuta ya petroli imepanda mara dufu, na kuongezea uzito wa mzigo unaozidi kulemea mlipa ushuru.

Hata hivyo, kwenye hotuba yake kwa taifa, Rais Kenyatta alisifia hatua ambazo alisema, serikali ilichukua mwaka wa 2020 na 2021 kuondoa na kupunguza ada na ushuru (VAT) kwa baadhi ya bidhaa muhimu za kimsingi.

Katika miezi ya karibuni utawala wa Kenyatta umekuwa ukikosolewa kwa kutokuwa na mikakati mahsusi ya kupunguzia wananchi mzigo wa ongezeko la gharama ya maisha, huku baadhi ya wakosoaji wakisema mikopo ya kimataifa ambayo serikali imechukua, imeathiri pakubwa uwezo wa serikali, kushughulikia maslahi ya wananchi.

TANZANIA

Nchini Tanzania, Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Nchini (Tucta) limetoa wito kwa rais wa nchi hiyo, Samia Suluhu Hassan, kutimiza ahadi yake ya kuongeza mishahara kwa wafanyakazi wa umma na kupendekeza kima cha chini cha mshahara kwa sekta zote kiwe Sh1, 010,000 milioni.

Akizungumza wakati wa sherehe za siku ya wafanyakazi katika uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma, Katibu Mkuu wa Tucta, Henry Mkunda, amesema kwamba tafiti zimeonyesha kuwa , ili kumwezesha mfanyakazi kuishi maisha bora, itabidi kiwango cha mishahara kiongezwe mara dufu.

Amesema wafanyakazi hawajaongezwa mishahara kwa takribani miaka sita kwa sekta ya umma na miaka tisa kwa sekta binafsi, na kwamba hali hiyo imesababisha kupungua kwa ari ya kufanya kazi, hivyo kupunguza ufanisi na uwajibikaji na tija mahali pa kazi, na kuathiri uchumi wa nchi.

Kwa sasa mshahara wa kima cha chini kwa sekta binafsi nchini Tanzania ni kati ya Sh40,000 na Sh60,00 kwa mfanyakazi wa nyumbani wakati kwa wafanyakazi wa mashambani na viwandani ni Sh100,000, kwa mujibua wa takwimu za serikali, kufuatia tangazo la mwaka 2013 katika gazeti la Serikali. Kima cha chini cha mishahara katika sekta ya umma, kilichotangazwa na serikali mnamo mwaka wa 2015 ni Sh300,000.

Baadhi ya wafanyakazi na familia zao nchini Tanzania wamekuwa wakilalamikia kupanda kwa gharama ya maisha hususan kufuatia janga la Corona, na vita vya Russia nchini Ukraine .

XS
SM
MD
LG