Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Aprili 18, 2024 Local time: 13:18

Kenya yashambulia maeneo ya al-Shabab


Helikopta za jeshi la anga la Kenya
Helikopta za jeshi la anga la Kenya

Kenya imefanya mashambulizi ya anga dhidi ya maeneo ya wanamgambo wa al-Shabab ndani ya Somalia kufuatia shambulizi lililouwa watu 148 katika Chuo Kikuu cha Garissa wiki iliyopita.

Msemaji wa jeshi la Kenya, Kanali David Obonyo, amesema walishambulia maeneo yanayojulikana kuwa ya al-Shabab Jumapili mchana na Jumatatu asubuhi.

Al-Shabab kundi la kigaidi la Somalia lilidai kuhusika katika shambulizi la Garissa Alhamisi ingawa washambulizi wao wote wanne waliuawa katika shambulizi hilo.

Wakati huo huo, Rais wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud amesema kundi la al-Shabab ni adui wa eneo zima la Afrika Mashariki na ni lazima likabiliwe.

FILE - Somalia President Hassan Sheikh Mohamud.
FILE - Somalia President Hassan Sheikh Mohamud.

Akizungumza katika mahojiano maalum na Idhaa ya Kisomali ya VOA siku tatu baada ya shambulizi la Garissa Rais Mohamud alieleza kusikitishwa kwake na shambulizi hilo. Alisema nia ya al-Shabab ya kulenga zaidi wakristo nchini Kenya ni kutaka kusababisha mtengano baina ya wakristo na waislamu nchini humo, lakini aliongeza kuwa shabaha yao hiyo imeshindwa kwa sababu Wakenya wanaelewa mbinu za magaidi hao.

Rais huyo wa Somalia anasema amezungumza na viongozi wa Kenya na kuwahimiza Wakenya kuungana katika kupambana na al-Shabab. Rais Mohamud alisema kundi hilo ni "adui asie na heshima."

Alipoulizwa kwa nini mashambulizi ya al-Shabab yameongezeka Kenya katika miezi ya karibuni, na endapo Kenya imejifunza chochote kutokana na mashambulizi hayo, rais huyo wa Somalia alisema al-Shabab haina uwezo wa kushambulia maeneo ya jeshi au serikali, ndio sababu sasa inashambulia maeneo ya raia ambayo ni rahisi kuyafikia.

Alisema mbinu hiyo inaonyesha kuwa kundi hilo linatapatapa na linakaribia kufikia mwisho.

XS
SM
MD
LG