Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Oktoba 11, 2024 Local time: 03:20

Kenya: Wanawake wakabiliwa na changamoto mpya kutokana na sheria mpya ya fedha


ETHIOPIA-AFRICA-AU-DIPLOMACY
ETHIOPIA-AFRICA-AU-DIPLOMACY

Wachambuzi wa masuala ya wanawake na uchumi wanasema Hali ngumu ya maisha na kupanda kwa bei ya mafuta  kufikia asili mia 16 kutoka asili mia 8 chini ya sheria mpya ya fedha ya serikali ya Kenya inazusha changamoto mpya kwa wanawake.

Wanawake wachache wanaohusika katika sekta ya uvuvi wanaiomba serikali kuwasaidia ili kuweza kukabiliana na mazingira mapya ya kazi zao.

Shughuli ya Uvuvi tangu jadi ni moja wapo ya sekta za kazi inayohusishwa wanaume pekee yao.

Lakini hali hiyo imekuwa ikibadilika pole pole katika pwani ya Kenya ambako baadhi ya wanawake wameanza kujihusisha katika fani hiyo ili kutafuta maisha bora.

Uvuvi

Wanawake wengine wanamiliki boti na kuajiri wanaume kwenda kuvua. Wanawake hawa pia ni wafanyabiashara wa samaki, wengine wanajishughulisha na usindikaji na biashara ya samaki: wananunua samaki kutoka kwa wavuvi, wanapika na kuuza kwenye migahawa au barabara za mijini

Rukia Mwanajuma ni mama wa makamo, yeye na wenzake wameungana katika kikundi cha wanawake 30 kuendeleza biashara ya Samaki mjini Kilifi katika pwani ya Kenya.

Bi Mwanajuma anaelezea zaidi, “nilikaa na kina mama wenzangu nikawashauri, wakatukabidhi hicho chombo, twashukuru, chombo kinapata samaki tuliajiri wavuvi wetu sisi kama kina mama na hao wavuvi wanakwenda baharini wakienda wakikesha wakituletea samaki,kama maji ni ya mchana wanakwenda kuchukua samaki wa juu wanakuja kutuletea sisi kina mama na tumeendelea kuwekeza hizo pesa kwa akaunti, tumefungua akaunt yetu.”

Biashara ya Samaki

Biashara ya Samaki inatoa fursa ya ajira kwa Mama Rahma na takriban asilimia 20 ya wanawake wengine nchini Kenya wanategemea uchumi wa baharini.

…Hatua Hii ya kujiajiri ni nafuu kwao kwasababu ya kiwango cha chini cha mtaji unao hitajika kuanzisha biashara ukilinganisha na fursa nyingine za biashara zilizopo kwa wanawake.

Licha ya fursa hiyo ya mapato, wanawake hawa wanakabiliwa na hatari ya manyanyaso kutoka kwa wavuvi wanaume kulingana na ripoti za vyombo vya habari na mashirika mbali mbali ya kutetea haki za wanawake.

Kutokana na uhaba wa samaki na bila ya kuwa na makubaliano maalum na mvuvi ni vigumu kununua samaki kwenye maeneo ya kutua kwa mashua.\

Wavuvi wanatumia fursa hii kuwanyanyasa. Haya na mengine mengi ni changamoto zinazotajwa kuwazuia wanawake kuaendelea kufanya kazi katika sekta hiyo.

Kando na hayo, takriban miaka kumi hivi katika biiashara hiyo ya kununua na kuuza samaki imepata pigo la kupungua kwa mazao ya baharini na kupanda kwa bei za bidhaa nchini Kenya.

Zaidi ya hilo wanawake hawa na wengine wanaotegemea sekta hii nchini humo sasa wanatabiri athari zaidi kufuatia ongezeko la bei ya mafuta ya petroli kwa asilimia 4 zaidi katika mwaka mpya wa fedha Kenya. Kupanda kwa mafuta ya petroli ambayo hutumika kuendesha boti za kuvua samaki imechangia kupanda kwa bei ya samaki wanaonunuliwa ndani na nje ya nchi.

Mgeni Abdalla ni mama muuzaji samaki anasema, “mimi siishi bila biashara ya uvuvi, mvuvi atoke baharini na pweza na mimi nije nipate au atoke baharini na samaki na mimi ndio nipate, nilikuwa nikinunua pweza kwa shilingi 150 lakini hivi sasa nanunua pweza 450 kwa kilo, nikiongeza gharama ya mafuta kilo 250 hizo zimekuja ngapi, 650, sasa, katika kilo moja hiyo 650 nifanye juhudi zangu inavyowezekana nipate na faida hapo. Kwahivyo mimi gharama naona iko juu mno kulingana na maisha yangu.”

Wanawake hawa katika Sekta ya Uvuvi sasa wanatoa wito wa msaada kutoka Kwa Serikali na kutafuta mbinu za kuwasaidia kukabiliana na gharama ya juu ya maisha wanayoendelea kushuhudia

Cha mno pia wanahofia kuangamia kwa biashara wanayotegemea kwasababu mwelekeo mpya unahatarisha kupungua kwa idadi ya wateja watakaoshindwa kuhimili kupanda kwa bei ya samaki kwa zaidi ya asilimia 50.

Biashara ya Kuuza Chakula

Saida Mwakaka anajishughulisha na biashara ya kuuza chakula ambayo inajulikana kama Mama Ntilie nchini kenya.

Saida Mwakaka anasema, “nilikuwa nanunua mfuko wa unga 80 bob kilo mbili sasa nanunua mfuko wa unga 240 au 250 mara tatu ya ile pesa nilikuwa nanunua mwanzo na sisi tuna watoto twasomesha, tuna mikopo twachukua pia,nina wenzangu kama wawili, watatu nawaajiri, yule mwenzangu aweza kosa ajira kutokea kwangu mimi kwasababu ya nini, hali ngumu ya uchumi ilivyo.”

Wataalam wa uchumi wanashauri kuwa changamoto nyingi zinazowakabili wanawake wafanyi biashara katika Sekta ya Uvuvi zinaweza kutatuliwa kupitia uingiliaji madhubuti wa utekelezaji wa Sekta hiyo, Aidha wanahitaji kuimarisha uwekezaji wao wa kibinadamu na kifedha katika sekta hiyo inayowafaidi wanawake ili waweze kuchukua jukumu muhimu zaidi katika biashara ya samaki na usindikaji.

Salma Mohammed, VOA Mombasa

Forum

XS
SM
MD
LG