Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Aprili 19, 2024 Local time: 09:19

Hatimaye Wamakonde Kenya wawezeshwa kupiga kura


Thomas Nguli mwenyekiti wa jamii ya Makonde Kenya akipongeza kutambuliwa kwa jamii yake kama raia wa nchi hiyo
Thomas Nguli mwenyekiti wa jamii ya Makonde Kenya akipongeza kutambuliwa kwa jamii yake kama raia wa nchi hiyo

Hatimaye jamii ya wamakonde imekuwa ni kabila la 43 nchini Kenya na kwa mara ya kwanza litashiriki katika Uchaguzi Mkuu mwaka huu.

Kitu ambacho kimewapa moyo watu wa kabila hili ni baada ya safari ndefu ya kutafuta haki zao za kupiga kura, mwaka huu kwa mara ya kwanza watashiriki uchaguzi mkuu Agosti.

Uhuru Kenyatta

Rais Uhuru Kenyatta
Rais Uhuru Kenyatta

Akiwakabidhi zaidi ya wamakonde elfu 4 vyeti vya uraia, vitambulisho vya kitaifa na vyeti vya kuzaliwa, rais Uhuru Kenyatta amesema jamii hiyo kwa sasa itashirikishwa katika maendeleo na ajira zinazotolewa na serikali ikiwemo vikosi vya usalama.

Wananchi hawa baada ya kupokea vyeti vya uraia na vitambulisho vya kitaifa na kadi za kupiga kura hawatakuwa tena na pingamizi ya kushiriki katika mchakato wa kidemokrasia wa kutafuta viongozi wao.

Maelfu waridhika

Kwa mujibu wa mwandishi wetu hatua hii imewafurahisha zaidi ya wamakonde elfu 4 wanaoishi nchini Kenya, baada ya serikali kuwapa vitambulisho na vyeti vya uraia.

Mama Amina Kassim Magoma pamoja na wenzake hawakuficha furaha yao huku wakiahidi kuiunga mkono serikali katika uchaguzi mkuu mwaka huu.

Hii ni baada ya shughuli ya usajili wa jamii hiyo inayojumuisha kabila la 43 nchini Kenya, iliyofanyika mwezi Oktoba mwaka jana kufuatia maandamano ya jamii hiyo kutaka uraia katika ikulu ya rais jijini Nairobi.

Uhuru Kenyatta akimtizama mama wa jamii ya Wamakonde akionesha kitambulisho chake
Uhuru Kenyatta akimtizama mama wa jamii ya Wamakonde akionesha kitambulisho chake

Amwagiza waziri

Mwandishi wa VOA mjini Mombasa anasema rais Uhuru Kenyatta amemwagiza Waziri wa Usalama wa Ndani kushughulikia suala la uraia wa makabila yalikuwa bado hayatambuliwi.

Hata hivyo jamii za warundi, wapemba na wanyarwanda walioshiriki maandamano ya kutafuta uraia pamoja na wamakonde siku za nyuma wamelalamika kuwa zoezi hili la usajili limewatenga.

Mama Mrundi akiomba serikali imsaidiye kupata kibali cha kuishi
please wait

No media source currently available

0:00 0:00:53 0:00

Mzee Julius Kiza na mama Stella Kilinga hawakuficha ghadhabu zao wakisikitika kwamba wao hawakuingizwa katika mchakato huo.

Lakini viongozi wa kisiasa kusini mwa pwani ya Kenya wanakoishi wapemba wengi wakiwa katika shughuli za uvuvi wameiomba serikali kusikiliza kilio cha jamii hiyo.

Imetayarishwa na mwandishi wetu Amina Chombo, Kenya.

XS
SM
MD
LG