Kutokana na hali hiyo serikali ya Kenya imeongeza vituo vya muda kuwaandikisha wapiga-kura, ambapo maafisa wa uchaguzi wanaendelea na zoezi la kuzuru sehemu mbali mbali ilikuwafikia wananchi.
Wachambuzi wa mambo ya kisiasa wanasema kuwa licha ya Kenya kuwa ni taifa lenye watu zaidi ya milioni 43 lakini bado idadi ndogo mno imejitokeza kujiandikisha.
Mwandishi wa Idhaa ya Kiswahili VOA amesema kuwa sasa kuna ushindani mkubwa baina ya chama tawala –Jubilee na muungano wa Upinzani katika harakati za kupata wafuasi wengi zaidi, tayari kwa maadalizi ya uchaguzi mkuu unaotarajiwa Agosti mwaka huu.
Katika mji wa Mombasa huko Kenya muungano wa upinzani umeweka kambi eneo la pwani ukiendelea kuwashawishi wafuasi wao kujiandikisha ili waweze kupiga kura.
Kinara wa upinzani Raila Odinga alihutubia maelfu ya wafuasi hao katika miji kadhaa huko Pwani. Bwana Raila alikubaliana na rais Uhuru Kenyatta kuwa zoezi la kuwapa raia vitambulisho linastahili kufanyika kwa haraka ili walio na vitambulisho waweze kujiandikisha kupiga kura.
Naye rais Kenyatta akiwa eneo la mashariki mwa Kenya aliongoza kampeni kama hiyo ya kuwarai wafuasi wa muungano wa chama cha Jubilee kujiandikisha kwa wingi.
Mkutano baina ya maafisa wa tume ya uchaguzi na wakuu wa utawala wa kaunti uliandaliwa mjini Mombasa kutangaza uzinduzi wa vituo vya muda vya kuwapa vitambulisho raia zaidi, na kuwandikisha vituoni ili kuwa wapiga kura.
Kamishna wa kaunti ya Mombasa Evans Achoki aliiambia sauti ya Amerika kuwa vituo hivyo vya muda vilivyofunguliwa ni juhudi ya serikali kuhakikisha kuwa kila mkenya aliyehitimu anapata haki ya kusajiliwa na kupata kitambulisho cha kitaifa.
Tahadhari ya Usalama
Wakati huo huo Serikali ya Kenya imeendelea kutoa tahadhari za usalama kupitia idara mbalimbali katika hatua za maandalizi ya uchaguzi.
Hii ni kutokana na Kenya kukumbwa na uvunjifu wa amani katika chaguzi za miaka ya nyuma.
Ttahadhari hii imechukuliwa kutokana na kukumbwa na mizozo, huku ikiaminika kuwa migogoro hiyo ilitokana na matamshi ya uchochezi kutoka kwa wanasiasa.
Tume ya utangamano na uwiano wa kitaifa NCIC iliundwa ili kushughulikia suala hilo, na sasa imejiandaa na mbinu mpya za kukomesha tabia hiyo.
Imeandaliwa na Waandishi wa Idhaa ya Kiswahili VOA Josephat Kioko, na Salma Mohamed, Kenya