Marais hao wamesema kuwa biashara iliyoko inafanyika bila vikwazo vyovyote na hivyo kuagiza tofauti zilizojitokeza katika baadhi ya bidhaa zimalizwe.
"Kuna mambo madogo madogo yanajitokeza katika biashara kati ya Kenya na Tanzania, tunataka kwa haya yote Mawaziri wa Kenya na Mawaziri wa Tanzania mkae myatatue, sisi hatuna tatizo, mambo mengine madogo madogo mno, mambo ya viatu, nguo, ngano, gesi ni madogo sana, mnatakiwa myatatue nyinyi yasifike kwetu, sisi huku tuko sawa sawa" amesema Dkt Magufuli, tamko ambalo limeungwa mkono na Rais Kenyatta.
Mazungumzo hayo yamejiri baada ya kukutana nchini Uganda ambapo Rais Uhuru Kenyatta na Rais John Magufuli wamewaagiza mawaziri wao kuyatafutia ufumbuzi masuala yenye kero ndogo ndogo ambazo hujitokeza kwenye maeneo ya biashara kati ya nchi hizo.
Marais hao walikutana Munyonyo mjini Kampala muda mfupi kabla ya kuanza kwa vikao vya mkutano wa wakuu wa nchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Kwa mujibu wa vyanzo vya habari nchini Uganda uhusiano baina ya mataifa haya mawili ulikuwa unalegalega katika wiki chache zilizopita baada ya Tanzania kuwakamata na kuwateketeza vifaranga kutoka Kenya.
Pia Kenya ilikerwa na tukio la Tanzania kupiga mnada mifugo iliyokuwa imevuka mpaka kuja nchini Tanzania kutafuta malisho.
Viongozi hao wametaka biashara inayofanyika tayari kati ya Tanzania na Kenya iendelezwe kwani kuna ishara za kutosha ambazo zinaonyesha kuwa inazidi kukua na bidhaa zinauzwa na kununuliwa baina ya nchi hizo.